• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 25, 2017

  HIMID MAO AWATUMIA SALAMU MSIMBAZI; AWAAMBIA...

  Na Mwandishi Wetu,  DAR ES SALAAM
  NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, ameweka wazi kuwa wana morali kubwa ya kupata matokeo mazuri katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) dhidi ya Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo, ambapo tayari kimeshaingia kambini tokea jana katika makao makuu ya klabu hiyo ndani ya viunga vya Azam Complex kujiandaa na mchezo.
  Himid amesema kwamba kikosi hicho kipo vizuri na watanufaika na urejeo wa wachezaji wao muhimu waliokuwa majeruhi, akiwemo Nahodha John Bocco.
  Kiungo wa Azam FC, Himid Mao kushoto amewatumia salamu Simba SC
  “Morali iko juu, timu ipo vizuri bahati nzuri wachezaji wenzetu karibia asilimia 90 wapo vizuri na wapo fiti na wako tayari kwa mchezo na naamini kocha atakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua timu yake ya kwenda kucheza mchezo huo,” alisema.
  Kiungo huyo anayesifika kwa ukabaji na mwenye mashuti makali, aliongeza kuwa mchezo huo utakuwa mgumu licha ya kufanikiwa kuwafunga mara mbili katika mechi mbili zilizopita.
  “Usidhani kama mchezo huu wa tatu utakuwa mrahisi kama mara mbili zilizopita tulizoshinda, kwani Simba nayo inajipanga, lakini naamini sisi tutajipanga vizuri zaidi ili kuweza kushinda mechi hiyo inayokuja,” alisema.
  Himid ambaye amekulia kwenye timu hiyo kwa takribani miaka tisa sasa, alitoa wito kwa mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuwapa sapoti kwani wao ni sehemu muhimu sana katika timu na uwepo wao utawaongezea nguvu zaidi uwanjani ya kuibuka kidedea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HIMID MAO AWATUMIA SALAMU MSIMBAZI; AWAAMBIA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top