• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 23, 2017

  TOTO YAENDA GEITA ‘KUTAFUTA DAWA’ YA KUBAKI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KATIKA kujiandaa na mechi zake za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Toto Africans ya Mwanza ipo ziarani mkoani Geita kwa michezo ya kirafiki.
  Ofisa Habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet aliiambia Bin Zubeiry Sports – Online jana kwamba jana walicheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Katoro Kids na kuibuka na ushindi wa 1-0, bao pekee la Mussa Mohammed.
  Japhet amesema timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Kishamapanda, Mwanza leo itacheza mechi yake ya pili ya kujipima nguvu dhidi ya Buseresere FC na mechi zote zinapigwa Uwanja wa CCM Katoro.
  Toto ambayo mchezo wake wa mwisho wa Ligi Kuu ililazimishwa sare ya 0-0 na Simba SC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ipo kwenye hatari ya kushuka Daraja hadi sasa ikiwa inashika na pointi 24 za mechi 26.
  Toto inalingana kwa pointi na JKT Ruvu ya Dar es Salaam na Maji Maji ya Songea ambazo kwa pamoja zinashika tatu za mkiani katika Ligi Kuu ya timu 16 baada ya kucheza mechi 27.
  Bahati mbaya zaidi katika mechi nne zilizobaki za Toto, watacheza na ‘baba zao’ Yanga SC ambao katika kampeni yao ya kutetea ubingwa wanatakiwa kushinda mechi zao zote zilizobaki.
  Mechi nyingine za Toto zilizobaki ni dhidi ya JKT Ruvu mjini Mwanza, Mtibwa Sugar mjini Morogoro na Azam FC Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TOTO YAENDA GEITA ‘KUTAFUTA DAWA’ YA KUBAKI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top