• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 27, 2017

  MKEMI APANDISHWA KAMATI YA NIDHAMU KWA ‘KUWACHANA’ SAA 72

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BODI ya Ligi Tanzania imemfungulia mashitaka Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi mbele ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Taarifa ya Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi leo, Boniface Wambura imesema kwamba Mkemi aliishutumu na kuidhalilisha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, ijulikanayo kama Kamati ya Saa 72 kupitia vyombo vya Habari kwamba inaendeshwa kiunaza na imegubikwa na rushwa.
  Wambura amesema Mkemi aliishitumu Kamati ya Saa 72 ambayo inafanya kazi kwa mwongozo wa Bodi ya Ligi kwamba iliamua suala la kadi tatu za njano za mchezaji Mohammed Fakhi Gharib wa Kagera Sugar kwa upendeleo kutokana na rushwa waliyopewa na Simba SC.
  Salum Mkemi (kulia) atapandishwa Kamati ya Nidhamu ya TFF
  “Mbali ya Kamati, shutuma hizo pia alizielekeza kwa TFF na kuwa tayari amekwisharipoti suala hilo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuwachunguza viongozi wa Kamati hiyo na TFF,”imesema taarifa ya Wambura.
  Aidha, Wambura amesema madai ya Mkemi si ya kweli bali yalikuwa yana lengo la kuwakashifu na kuwadhalilisha viongozi wa TFF na Kamati ya Saa 72 mbele ya mashabiki wa mpira miguu na Watanzania kwa ujumla.
  “Kutokana na kitendo hicho ambacho kina lengo la kusababisha vurugu kwenye mpira wa miguu, tunaomba mlalamikiwa aadhibiwe kwa mujibu wa ibara ya 53 (1) na (2) ya kanuni za Nidhamu za TFF pamoja na kanuni ya 41 (2) ya Ligi Kuu,”amesema Wambura na kuongeza; “Pia apewe adhabu nyingine kama ambavyo Kamati ya Nidhamu itaona inafaa kwa kuzingatia Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012,”.    
  Mkemi kwa upande wake alisema hajapata barua rasmi ya Bodi juu ya wito huo na atakuwa tayari kulizungumzia hilo mara atakapopata barua hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MKEMI APANDISHWA KAMATI YA NIDHAMU KWA ‘KUWACHANA’ SAA 72 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top