• HABARI MPYA

    Friday, May 15, 2015

    BASATA NI KIBOGOYO, MALINZI WETU ANAKUMBATIA MIZOGA, STARS IMESHAHUKUMIWA KIFO, STAND IMEPANDA KIMIZENGWE, INABAKI KIMIZENGWE

    Hemed Kivuyo, DAR ES SALAAM
    MIMI ni Mpenzi wa Muziku wa Taarab za zamani zilizonizidi Umri, za akina Malika, Mwanahela, Shakila, Aly mtoto Sefu, Bi Mtumwa na wengineo.
    Kuna Wimbo mmoja katika moja ya Shairi lake linasema hivi..’Bunduki bila Risasi yaua namna Gani? Yaua namna gani Bunduki Bila Risasi?) Ni Maneno machache yaliyovikwa Nguo nakuhitaji kufikirisha akili kung’amua. Unaweza Kumiliki Bunduki, lakini haina Risasi (Nitafafanua mbele ya Makala haya)
    Nakumbuka nilipokuwa darasa la sita siku moja Nyakati za Usiku wasaa nne hivi, Nyumba ya Jirani kukatokea Msiba, Baba Yangu Mkubwa ( Ally) alienda Msibani nami niliongozana naye kwa kuwa haikua mbali na Tunapoishi. Ilitulazimu kuruka `mfereji` mmoja Ndipo tufikie Nyumba ya Msiba,kabla yakufikia mtaro huo kulikuwa na wadudu wanaolia hasa Nyakati za usiku,,chrii,,chrii,,chrii,,.tulipofika jirani kabisa na mfereji  huo wale wadudu wakaacha kulia. wakawa kimya.
    Wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania wakiwa mazoezini leo mjini Rustenburg, Afrika Kusini

    Tulipovuka kama hatua tano hivi Baba Mkubwa akanambia hebu tusimame, Tuliposimama kwa sekunde kadhaa wale wadudu wakaanza kulia tena..chriii,,chriii,,chrii.
    BABA Mkubwa akanambia unasikia hao wadudu wanaolia! Siku Nyingine hata ukiwa porini ukivuka mto usiku utasikia hao wadudu wananyamaza na ukimaliza kupita wataanza kulia tena. Akanambia kama hutowasikia wakilia basi ujue kuna mtu anakufuata Nyuma na uchukue tahadhari. Kwakuwa wadudu hao wakisikia kishindo tu wananyama.
    RAIS wa TFF Gamal Malinzi amevuka Mfereji wale wadudu walinyamaza akiwa anavuka,ametembea hatua kadhaa  wale wadudu bado wamenyamaza ,Gamal Malinzi hachukui tahadhari. Ngoja nimpigie Simu Baba Yangu Mkubwa anambie nini kitampata Gamal Malinzi baada ya kupuuzia ishara hiyo.
    Siku moja nilikuwa Kijiweni kwetu tukawa tunapiga `story` za Soka letu hapa Nchini ,nikawa nawaambia jamaa zangu `jamani huyu Rais Malinzi ni Mtu safi jamani tumpe muda atatufikisha katika Nchi ya Maziwa na asali,. Jamaa walinigeuka vibaya wakaanza kunitupia maneno magumu nayasiyovikwa Nguo.
    Nikaawaambia jamani huyu Malinzi ana nia Njema ni mpole,ni mtu wa watu na anakerwa na afya mbovu ya Timu yetu ya Taifa,wakanambia niondoe ujinga wangu huko!!  Sikukata tamaa  nikawaambia huyu Rais alikuja na mambo mengi mazuri jamani,oneni alivyoleta Taifa Stars `maboresho` leo tungemwona wapi Said Juma `makap?  Angalieni Ofisi za TFF zinazokarabatiwa na kuleta heshima! Hamuoni?
    Jamaa mmoja akainuka kitini akaanza kunirarua kwa maneno akisema `wee vipi bwana! Umeona wapi mchezaji anachezea Timu ya Taifa bila kupitia Kilabu chochote? Huyu Mchezaji unamtoa Nanjilinji aje kupambana na Yaya Toure aliyecheza michezo 100 ya kimataifa? Hapo Nikakaa kimya.
    Mmoja akaibuka na kusema ``Kwanza huyu Rais anahusishwa na ile Timu ya Stand united iliyopanda daraja kimizengwe na ikabaki ligi kuu kimizengwe,. Hapo sikukubali nikainuka na mimi, kabla sijaongea mmoja akanambia ,,wacha ubishi wewe Jamaa anamkono wake Katika ile Timu.( sikuamini na wala siamini bhana)
    Wakanambia wewe ( RAIS MALINZI) umeandika historia hata kabla ya kumaliza muda wako kwa Ligi yetu kuendeshwa Kienyeji ,yaani eti Ligi inasimama na michezo kuahirishwa kwasababu dhaifu dhaifu na kutoa mwanya kwa Upangaji wa matokeo na kuwalinda watendaji Dhaifu.
    Nikakutetea sana Mh Malinzi lakini Nikashindwa Nguvu  ya Hoja . Wakazidi kuropoka  eti unafuatwa na `inzi` kwakuwa umekumbatia `mizoga` nikawauliza wanamaanisha nini? Mmoja akasema eti pale Ofisini kwako kuna baadhi ya wafanyakazi wanatafuna Fedha za Shirikisho kiholela lakini ukiambiwa huamini,huamini kwakuona wala kusikia.
    Eti wanasema ulipoingia Ofisini hukutana hata kutumia kiti kilichotumiwa na Mtangulizi wako na Ndiyo maana ukahamia `Mjini` lakini FIFA ikakurudisha na hata baadhi ya  wafanyakazi wa mtangulizi wako ukawafuta kazi `kiroho` mbaya.!!! Asee sikukubaliana nao.
    Wakasema eti mtindo mpya uliyotaka kuanzisha kutaka kukata makato ya vilabu ni kama `wizi` sijakubali hata kidogo Mh.Rais     
    Eti una mipango Mingi na Ndiyo maana huna chakujivunia mpaka sasa! Waliongea mengi mengine tukionana ntakwambia hayafai kuandika hapa, Nikaondoka nikawaacha wana`bwabwaja`.
    Nikaenda zangu mpaka kijiweni kingine ambacho wanakunywa `kahawa` nikakuta wanazungumzia Timu yetu ya Taifa. Taifa Stars, wanasema eti hii Timu sasa kama vile haina Mwenyewe,ameachiwa Kocha Nooj afanye anavyotaka,ateue wachezaji majeruhi,ateue wachezaji wanaokaa `benchi, kisha alipwe Fedha Nyingi.
    Nikawaangalia wale jamaa wakibwabwaja nao wakawa wanakuhusisha na uteuzi huo,sikuvumilia nikawavaa tena,nikawaambia `hivi         Nyie huyu Rais alaumiwe kwakipi? Wakanambia unapaswa kulaumiwa kuliko huyo Kocha Uliyemleta.
     Mmoja akasema ule Mpango wa kuweka watoto pamoja kwa zaidi ya miaka mitano ambayo kazi ukamwachia Adolph Rishedy ni moja kati ya `ablakadabra` unazoendelea nazo. Wakasema inawezekana uteuzi wa Risheedy ukawa ni sahihi lakini Mpango ni Mbovu.
    Wakasema eti hakuna kitu kama hicho ulimwenguni,wakahoji unamweka huyo mtoto mpaka afikishe umri wa miaka 18 na zaidi wakati huo wewe ukiendelea kuwa Rais? Wakati huo ukibaini mtoto huyo hakuwa na kipaji?  Rais ajaye akija na falsafa yake? Wakasema eti `ulikurupuka kama ulivyokurupuka` kuanzisha Taifa Stars Maboresho!! Sikukubali,nikamkunja mmoja shati,wakaanza kunivamia nikamwachia.
    Eti wanasema hata lile Basi la Timu ya Taifa liliwahi kukamatwa kwasababu ya Deni,nikawaambia hilo nitabisha mpaka Mwisho kwakuwa nina ushahidi,mmoja wao akanionyesha ka ushahidi kake,
    Mwehu mmoja akaanza kuropoka eti ``hata huyo anayekaimu Bodi ya Ligi hana uwezo ila unamlinda wewe! Nikahoji jamani anamlinda kivipi? Wakasema weeee,,inamaana hujui? Nikawaambia sijui nifafanulieni,Mwingie akasema eti Timu ya Taifa kwa michuano iliyopo mbele yake nikama imeshahukumiwa kifo tu, kabla sijajibiwa nikatimua mbiyo.
    Mh. Malinzi Bunduki Bila Risasi yaua namna gani??
    NDUGU MSOMAJI TANZANIA TUNAKABILIWA NA KADHIA TELE,TUNA RAIS WA NCHI AMBAYE ANAMALIZA MUDA WAKE LAKINI SISI WANAMICHEZO TUMESHINDWA KUMTUMIA VYEMA NA SASA ANAONDOKA, SIONI RAIS AJAYE ANAYEPENDA MICHEZO KAMA JAKAYA KIKWETE ANAYEONDOKA, TUMUOMBE RADHI .
    Wakati katika Muktadha wa Michezo tunakwenda kama kuku aliyekatwa kichwa, ukigeuka pembeni unaona BASATA ikiangalia msanii kama yule SHILOLE akitembea na kuimba uchi huku BASATA iliyokosa `MENO` ikiendelea kumkemea kwa kucheka. Taifa linaenda likivuliwa Nguo na walopewa dhamana kulivika Taifa Nguo `wanachekacheka tu`. Napata `kizunguzungu`. WACHENI NIZUNGUMZE KAMA MWENDAWAZIMU.
    Wakati wa Mwl. Nyerere angalau maadili yalitamalaki! Huyu SHILOLE yeye ni nani achafue hali ya hewa kiasi hiki? BASATA badala ya kukemea na kuchukua hatua inakuwa kama `mlezi wa tabia mbovu?

    (Mwandishi wa makala haya ni Mtangazaji wa Redio One na ITV, ambaye anapatikana kwa namba +255 655 250157 na +255 752 250157) 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BASATA NI KIBOGOYO, MALINZI WETU ANAKUMBATIA MIZOGA, STARS IMESHAHUKUMIWA KIFO, STAND IMEPANDA KIMIZENGWE, INABAKI KIMIZENGWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top