• HABARI MPYA

    Thursday, November 06, 2014

    UNAZI PEMBENI; VIONGOZI WA SIMBA SC MNATUBOA, ZINDUKENI, ACHENI UZAMANI!

    Na Kivamwo, A Simon, DAR ES SALAAM
    HAMKANI hali si shwari katika klabu yetu ya Simba SC ukipenda iite Wekundu wa Msimbazi. Pamoja na kwamba kwa miaka mitatu timu yetu haijafanya vizuri lakini kinachotokea sasa katika klabu yetu ni ukosefu wa umakini na kutokwenda na wakati kwa viongozi wetu wapya wakiongozwa na Rais Evans Aveva na makamu wake Bw.Nyange Kaburu. Kwa maana nyingine viongozi hao wameingia madarakani wakiwa na "hangovers" za miaka ya nyuma walipokuwa katika kundi la Friends of Simba (FoS). Kipindi walichojizolea umaarufu wa kuusaidia uongozi wa akina Mzee Hassani Dalali na Mwina Kaduguda kuiwezesha Simba kufanya makubwa katika medani za kitaifa na kimataifa. Ukumbuke kipindi hicho ndipo waliiwezesha Simba kuitoa timu ngumu enzi hizo ya Zamalek ya Misri. Hayo yalishapita na yamebaki historia. Lakini pia hawajastuka kuwa mazingira ya soka la Bongo yanabadilika na kuchukua sura mpya kabisaa.
    Mwenyekiti wa Simba SC, Evans Aveva wakati wa kampeni za kuomba uongozi Simba SC aliahidi pointi tatu, kwa maana ya ushindi, lakini timuimetoa sare sita katika mechi zake zote za mwanzo Ligi Kuu

    KUZEMBEA NA KUWAACHIA WACHEZAJI KUHAMIA TIMU NYINGINE: 
    Hili ndilo kosa kubwa uongozi wa Simba umekuwa ukifanya kwatakribani miaka minne au mitano iliyopita. Kujifanya eti wao ni chuo cha wachezaji na kuwauza kokote iwe Yanga au timu nyingine. Hili limeigharimu klabu ile mbaya. Hawalioni au hawataki kulikubali lakini, huu ndio mwanzo wa Simba kuanza kupepesuka. Na ni mzimu mbaya mno unaoitafuna klabu yetu.nani anabisha kuwa wachezaji wote waliotemwa Simba ama kwa mizengwe au uzembe wa viongozi wetu sasa kule waliko ni moto wa kuotea mbali? Mfano: Kelvin Yondani, Aziz Gilla, Musa Hassani Mgosi, Deo Munishi, Mustafer Bartezi, Danny Mrwanda, Shomari Kapombe, Salum Kanoni, Juma K Juma, Moshi Boban, Stephen Mazanda wa Mbeya City, etc...angalia hata Emmanuel Okwi alivyokuwa ameuzwa kwa uzembe usiokuwa na kipimo?. Sasa fikiria uongozi wa sasa bila hata haya, soni, wala aibu, unataka kumwachia Amiss Tambwe-mfungaji bora wa msimu uliopita eti aondoke. Kina Mkude, Singano, Chanongo, Kiemba nao eti wanapewa uhuru wa kuondoka kama wanataka...kha? jamani?? huu si ni ukosefu wa umakini uliopitiliza mipaka? Nani hajui Tambwe alivyokuwa anacheka na nyavu kila siku msimu uliopita?. Uongozi unakosa sera za Staff (Players) Retaining?? --hebu jikumbushe jinsi alivyotemwa kiurahisi na uzembe usiokuwa na mfano jembe letu Donati Musoti (Soldier)..nani alikuwa hajui shughuli ya beki yule akiwa uwanjani. Sasa leo umewapandisha wale mayanki toka kikosi B ambao hawajawa na uzoefu wa mikiki mikiki ya ligi wakitoka sare unawalaumu eti wanahujumu. Mara ooh, hawajitumi? nani kasema bwana?. Zamani tukiwa bado wadogo, aisee, ilikuwa shughuli kumruhusu mchezaji atoke Simba kwenda Yanga ama kinyume chake. Yanga hadi leo wamekomaa na msimamo huo, na kwa kiasi kikubwa msimamo huo unawasaidia kwani timu unakuta ina wachezaji maveteran (wakongwe) na wenye uwezo wa kubadili matokeo pale inapobidi.
    Kocha Patrick Phiri wa pili kulia akisaini Mkataba na Aveva. Mzambia huyo sasa anaweza kufukuzwa baada ya mechi Jumapili asiposhinda 

    KOCHA PHIRI: Hakuna asiyeujua uwezo wa kocha patrick Phiri. Leo uongozi kwa kutojua ulipojikwaa unataka kumtimua kwa kumpa mechi mbili asitoke sare wakati wao wenyewe ndio wamemkabidhi timu changa ambayo hakuhusika kuisuka. Hebu mtimueni Phiri muone kitakachotokea kama sio kusambaratisha hata hicho kidogo alichokuwa amekiunda
    Ndanda FC ilipanda tu Ligi Kuu na kukutana na udhamini wa Bin Slum

    UDHAMINI WA AZAM TV NA VODACOM ETC: 
    Uongozi wetu unashindwa kung'amua kuwa hali ya ushindani miongoni mwa timu za VPL ime-change sana ikichangiwa na udhamini kwa vilabu toka kwa wadau mbali mbali, mf Azam TV, Vodacom, Binslum Tyres, Postal Bank, Cocacola etc. Kwa sasa kila mchezaji wa timu ya VPL ana uhakika wa mshahara na malupulupu kila mwezi. Pia ana mkataba. Yale mambo ya kujilegeza wanapokutana na timu za Simba na Yanga hayapo tena. Siku hizi wanakomaa ili kulinda kibarua. Hakuna cha timu ndogo kama ilivokuwa zamani. Waulizeni Yanga kilichowakuta juzi huko Kagera, au Azam FC huko Ndanda Kuchele...Mpira unachezwa hadharani na wote wanauona kupitia Azam TV au uwanjani tofauti na miaka ya nyuma, tulikuwa tunausikiliza RTD. anakwendaaaaa...goo..goo...hapana, penalt??..nini??..refa kapeta...teh teh..kumbe ni porojo na midadi tu ya mtangazaji. Siku hizi kila kitu kiko wazi, kinaonekana. Kwa hiyo kila mchezaji wa VPL anacheza kwa kujituma akijua hakuna longolongo lakini pia anatetea kibgarua chake.
    Kikosi cha Simba cha mwaka juzi, wachezaji kibao wameondoka. Haya ni makosa yanayoidhoofisha timu

    HITIMISHO: viongozi wa Simba tulieni, acheni kupanic na sare hizo, mwacheni kocha Phiri ajenge kikosi (mbona timu nzuri tu ile?), wasikilizeni wachezaji wanataka nini, wapeni haki zao, acheni kuwabagua...walipeni mishahara yao vema, hakikisheni mikataba yao iko sawasawa wasipate mawazo ya kuanza kuongea na vilabu vingine kwa mujibu wa sheria. Warejesheni wale wanachama 70 waliosimamishwa ingawa sikubaliani na madai ya watu eti hao jamaa (UKAWA) ndio wanaopelekea tutoke sare mfululizo. Mbona enzi za Rage walikuwepo kundini na kila siku sare na kufungwa vilitamalaki? nasema warudishwe kwa lengo la kuleta umoja wa klabu. Basi. Simba itarejea pahala pake. Leo nimejivua unazi nimevaa nguo rasmi. SIMBA NGUVU MOJA!!.
    (Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba ya simu 0713 300219).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UNAZI PEMBENI; VIONGOZI WA SIMBA SC MNATUBOA, ZINDUKENI, ACHENI UZAMANI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top