• HABARI MPYA

    Thursday, November 13, 2014

    MAXIMO AACHA AGIZO YANGA SC HAMISI KIIZA ATEMWE KATIKA USAJILI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mbrazil wa Yanga SC, Marcio Maximo amerejea nyumbani kwao kwa mapumziko mafupi, lakini ameacha pendekezo kwa uongozi, mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza aondolewe katika usajili.
    Hata hivyo, uongozi wa Yanga SC ni kama haujaafiki wazo hilo la kocha wao Mkuu, anayesaidiwa na Mbrazil mwenzake, Leonardo Leiva na kuna uwezekano mkubwa ‘Diego wa Kampala’ akaendelea kuwamo kikosini.
    “Maximo alipendekeza Kiiza aachwe, lakini wazo hilo hatujaliafiki, kuna sababu za msingi tumezingatia,”kimesema chanzo kutoka Yanga SC.
    Hamisi Kiiza hatakiwi na kocha Maximo Yanga SC

    Kiiza aliyekuwa mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita katika Ligi Kuu, msimu huu amejikuta anasotea namba kwenye kikosi cha kwanza chini ya Mbrazil huyo.
    Maximo alileta wachezaji wawili kutoka Brazil baada ya kutua Yanga SC Julai mwaka huu, kiungo Andrey Coutinho na mshambuliaji Genilson Santana Santos ‘Jaja’.
    Na ujio wa Wabrazil wenzake hao umemuondoa kabisa kwenye kikosi cha kwanza Kiiza, ambaye tangu amesajiliwa Yanga SC mwaka 2011 amekuwa akikubalika na makocha wote waliotangulia.  
    Kiiza alisajiliwa Yanga SC wakati wa kocha Mganda mwenzake, Sam Timbe, lakini akaendelea kuwa na nafasi kikosi cha kwanza hata kwa makocha waliofuatia, Mserbia Kosta Papic, Mbelgiji Tom Saintfiet na Waholanzi Ernie Brandts na Hans van der Pluijm. 
    Maximo amerejea Brazil, akitoa mapumziko ya wiki moja kwa timu nzima, kufuatia kusimama kwa muda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hadi mwishoni mwa Desemba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAXIMO AACHA AGIZO YANGA SC HAMISI KIIZA ATEMWE KATIKA USAJILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top