• HABARI MPYA

    Friday, November 14, 2014

    APR YATAKA KUWANG’OA YANGA SC NGASSA NA NIYONZIMA KWA GHARAMA ZOZOTE

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    APR ya Rwanda imempigia simu Mrisho Khalfan Ngassa kumuuliza juu ya Mkataba wake Yanga SC na kumuweka wazi kwamba inamtaka.
    “Ni kweli, APR wamewasiliana na mimi, wakauliza kuhusu mkataba wangu, lakini nikawaambia wawasiliane na klabu yangu,”amesema Ngassa akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni ya leo. 
    Ngassa amewajibu APR kwamba bado yupo ndani ya Mkataba na Yanga SC ambao haumruhusu kuingia kwenye majadiliano mengine ya kimkataba na klabu nyingine.
    Na APR ikamuambia wazi mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Simba SC, itafanya mawasiliano na Yanga SC juu ya uwezekano wa kumnunua haraka iwezekanavyo.
    Mrisho Ngassa (katikati) wakati akichezea Simba SC, akijaribu kupasua katikati ya wachezaji wa Yanga, Haruna Niyonzima kushoto na Didier Kavumbangu (sasa yupo Azam FC) kulia

    Inaonyesha APR ina taarifa nyingi kuhusu Ngassa na Yanga hadi suala la mchezaji huyo kuchukua mkopo benki kwa ajili ya kulipa deni la Simba SC.
    BIN ZUBEIRY inafahamu kwamba, baada ya Ngassa kusaini Mkataba wa miaka Yanga SC mwaka jana, akitokea Simba SC alipokuwa akicheza kwa mkopo kutoka Azam FC, alilipwa Milioni 80.
    Lakini baadaye, Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikajiridhisha Ngassa alisaini Mkataba mwingine Simba SC, hivyo akaamriwa kurejesha Sh. Milioni 35 na faini ya Sh. Milioni 10 kwa Wekundu wa Msimbazi.
    Yanga SC wakaamua kumuunganishia Ngassa mkopo wa Milioni 45 benki, alipe deni la SImba SC naye awe anakatwa katika mshahara wake kila mwezi- na deni hilo hadi sasa halijaisha na lipo katika mazingira ambayo mchezaji mwenyewe ‘haelewi elewi’.
    Timu hiyo ya Jeshi la Rwanda imeonyesha iko tayari kabisa kutatua tatizo la mkopo wa Ngassa benki na kuingia naye Mkataba akaanze kazi Kigali.
    Haruna Niyonzima naye kushoto anatakiwa arejee APR

    Mbali na Ngassa, habari zaidi zinasema APR wanamtaka pia na kiungo wao wa zamani, Haruna Niyonzima anayecheza Yanga SC kwa sasa, arejee nyumbani.
    Niyonzima aliyejiunga na Yanga SC mwaka 2011, kama Ngassa wote mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu, katikati ya mwaka ujao.
    Niyonzima tayari amewagomea Yanga SC kusaini Mkataba mpya, akisema anataka kuondoka Tanzania baada ya miaka minne ya kuwa kazini Dar es Salaam.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: APR YATAKA KUWANG’OA YANGA SC NGASSA NA NIYONZIMA KWA GHARAMA ZOZOTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top