• HABARI MPYA

    Saturday, October 11, 2014

    SAMATTA NA BOCCO WATAKOSEKANA KESHO STARS NA BENIN, NOOIJ ATATUMIA MABEKI WATATU…KWA MFUMO UPI?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WASHAMBULIAJI wawili, Mbwana Ally Samatta na John Raphael Bocco ambao Mholanzi Mart Nooij amekuwa akiwatumia katika mechi zilizopita kucheza pamoja na Thomas Emmanuel Ulimwengu watakosekana kesho kwa sababu wote ni majeruhi.
    Samatta amebaki Lubumbashi baada ya kuumia akiichezea klabu yake, Tout Puissant Mazembe katika Nusu Fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ES Setif ya Algeria. Mazembe ilitolewa kwa mabao ya ugenini, baada ya sare ya jumla ya 4-4. 
    Bocco wa Azam FC anaendelea kuuguza goti aliloumia Agosti kwenye Robo Fainali ya Kombe la Kagame, dhidi ya El Merreikh ya Sudan mjini Kigali, Rwanda. Azam ilitolewa kwa penalti.
    Kocha Mart Nooij atatumia mfumo gani mechi na Benin kesho?

    Maana yake, kama kocha huyo Mholanzi ataendelea kutumia mfumo wa 4-3-3 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kesho dhidi ya Benin, atalazimika kuwa na wachezaji wa kuziba pengo la wawili hao.
    Ameonekana ni muumini wa wachezaji wenye maumbo makubwa- na katika kikosi alichoteua zaidi ya Ulimwengu, anabaki na washambuliaji wengine wawili, Mwegane Yeya wa Mbeya City na Juma Luizo wa ZESCO United ya Zambia.
    Ni hao ambao watachukua nafasi za Samatta na Bocco, au kocha Nooij atabadili mfumo? Tutajua kesho.
    Kwa kuwa tayari Nooij amesema katika mchezo huo atatumia mabeki watatu wa kati, ili kuwa na ukuta mgumu, mmoja wao akicheza kama kiungo mkabaji ili kuwapunguzia wenzake majukumu- maana yake kuna uwezekano akatumia mfumo wa 4-4-2 kesho.
    Kama atacheza na wachezaji saba katika ukuta, basi atahitaji japo wachezaji wawili katikati ili kutengeneza uwiano kati ya nyuma na mbele- jambo ambalo linaleta picha ya kutokuwa na washambuliaji watatu kesho. 
    Kama baada ya ukuta wa watu saba atakuwa na viungo wengine wawili katikati- maana yake zitabaki nafasi mbili kwa ajili ya washambuliaji na viungo wa pembeni. Akiongeza kiungo mmoja atakuwa na nafasi tatu. Kuna shauku kubwa ya kutaka kujua kikosi cha Stars kitakuwaje kesho.
    Nooj amesema mpango wa kutumia mabeki watatu wa kati, unafuatia makosa yaliyofanywa na timu yake katika mechi ya mwisho dhidi ya Burundi ambayo ndani ya dakika 15 za kwanza walijikuta wanafungwa mabao mawili ya haraka haraka dakika ya kwanza na 12.
    Kwa ujumla, tangu ametua Stars Nooij ameiongoza Stars katika mechi nane na kati ya hizo, ameshinda mbili amefungwa tatu na kutoa sare tatu na katika mechi zote hizo nyavu za Stars zimetikiswa mara 12, huku yenyewe ikifunga mabao tisa.
    Mbwana Samatta (wa kwanza kulia) na John Bocco (wa kwanza kushoto waliosimama) watakosekana kesho Taifa Stars ikimenyana na Benin. Kikosi kitakuwaje?

    Bila shaka langoni ataendelea kusimama Deo Munishi ‘Dida’, beki ya kulia Shomary Kapombe, kushoto Oscar Joshua na katikati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan.
    Nani atakuwa beki wa tatu wa kati? Hilo ndilo swali kwa sababu katika mechi zilizopita amekuwa akimtumia Erasto Nyoni katika kiungo mkabaji, lakini kwa kupona Jonas Mkude maana yake anaweza kufanya mabadiliko.
    Na yatakuwa mabadiliko ambayo yatamfanya Nyoni arudi benchi au ndiyo akawe beki wa tatu wa kati? Said Mourad amekuwa akiingia kwenye mipango ya Nooij anapoamua kuongeza idadi ya mabeki- maana yake naye kesho na anafasi ya kuanza katika 11.
    Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amerudi katika fomu na viungo wengine Said Ndemla, Himid Mao na Amri Kiemba wote wapo vizuri, lakini Nooij amekuwa akimtumia Mwinyi Kazimoto kama kiungo mchezeshaji- kesho itakuwaje?
    Washambuliaji wa pembeni wote Mrisho Ngassa, Simon Msuva, Khamis Mcha ‘Vialli’ na Haroun Chanongo nao wapo vizuri maana yake katika mchezo huo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya FIFA wanaweza kucheza kwa zamu, lakini je akina nani wataanza?
    Katika jitihada za kuwa na kikosi cha uhakika, chenye wachezaji bora wa akiba, Nooij amewaita chipukizi beki wa kulia Miraj Adam, beki wa kushoto Edward Charles na beki wa kati Joram Mgeveke- nao bila shaka watapata nafasi kidogo kwenye mchezo wa kesho.
    Hivi sasa Nooij anajaribu kutengeneza timu ya kampeni za baadaye baada ya kukosa nafasi ya kwenda Morocco mwakani kwenye AFCON na mchezo wa kesho utakuwa hatua nzuri ya kuanzia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA NA BOCCO WATAKOSEKANA KESHO STARS NA BENIN, NOOIJ ATATUMIA MABEKI WATATU…KWA MFUMO UPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top