• HABARI MPYA

    Sunday, October 19, 2014

    RUSHWA NA UPANGAJI MATOKEO KATIKA MECHI SUMU YA SOKA YA TANZANIA, MALINZI KAZI KWAKE

    HAUJAWAHI kutolewa ushahidi wa kumtia mtu hatiani kwa kutoa, ama kupokea rushwa au kuhusika na njama za kupanga wa matokeo katika michezo ya soka nchini.
    Lakini tuhuma zimekuwa nyingi mno na kwa muda mrefu sasa, kwamba marefa na wachezaji wanahongwa ili kupanga matokeo.
    Kipa Shaaban Hassan Kado miaka minne iliyopita akiwa Mtibwa Sugar aliwahi kutoa madai ya kushawishiwa na mchezaji wa zamani wa Simba SC, Ulimboka Mwakingwe apokee rushwa ya kiongozi wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.

    Wakati huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lipo chini ya Rais Leodegar Tenga, tuhuma hizo zilizimika kama zilivyoibuka.
    Lakini bado tuhuma za rushwa na upangaji wa matokeo zimeendelea katika soka yetu, watuhumiwa wakuu wakiwa marefa na wachezaji.
    Hao wanatuhumiwa kuhongwa ili kutimiza masharti ya wanaowahonga, ambao ni viongozi wa klabu wanaotaka timu zao zishinde kwa urahisi.
    Klabu nchini zimekuwa zikifungia na kufukuza wachezaji wake, kwa madai walihujumu timu, yaani walipoka hongo kucheza chini ya kiwango timu zao zifungwe.
    Baada ya kuingia madarakani Oktoba mwaka jana, Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi moja ya ahadi zake ni kwamba atapambana na rushwa na upangaji matokeo.
    Tena Malinzi alisema kwa msistizo; “Nikimgundua mtu amehusika kupanga matokeo, ama zake ama zangu”.
    Hakika lilikuwa ni tamko zuri na la faraja kwa wapenda maendeleo katika soka ya nchi hii, kwa sababu mchezo huo hauishii tu kwenye kuzinufaisha timu zinazofanya hila hizo ili kushinda mechi, bali zinakwenda mbali zaidi kiasi cha kuathiri mno soka ya Tanzania.
    Tunakosa kujua wachezaji halisi bora, kwa sababu wanaoonekana wanafanya vizuri, hawapati ushindani unaostahili uwanjani.
    Kama kipa kahongwa afungishe, je, huyo mfungaji atasifiwa kwa lipi? Kama refa kahongwa aipendelee timu ishinde, je hiyo timu hata ikitwaa ubingwa, itakuwa na furaha gani?
    Lakini zaidi tunazinyima nafasi klabu na wachezaji bora kupata kile kinachostahili kwa sababu ya ujinga huo.
    Mchezaji amekuwa mfungaji bora, wakati mabao yake ni ya kuachiwa na safu za ulinzi za timu pinzani, au marefa kumruhusu kufunga akiwa ameotea, je hapo anaibiwa nani?
    Hali hii imekuwa ikiwafanya hadi makocha wa timu za taifa, wachague wachezaji ambao si bora tu kwa sababu wanafanya vizuri uwanjani- lakini kwa kutengenezewa mipango.
    Wachezaji ambao wanafanya kwa juhudi zao, lakini wanazidiwa na wale ambao wanatengenezewa mipango, wanakosa nafasi wanazostahili- ila mwisho wa siku inayoathirika ni soka ya Tanzania. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RUSHWA NA UPANGAJI MATOKEO KATIKA MECHI SUMU YA SOKA YA TANZANIA, MALINZI KAZI KWAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top