• HABARI MPYA

    Sunday, October 05, 2014

    NAMNA HII, TUNAWEZA KUONEKANA WEHU!

    MWAKA 2004 Tanzania ilifuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zilizofanyika Gambia mwaka 2005.
    Lakini kwa bahati mbaya, Tanzania haikwenda kwenye fainali hizo baada ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Tanzania ilifungiwa kwa sababu timu yake ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ilikutwa na hatia ya kutumia mchezaji aliyezidi umri, Nurdin Hamad Bakari wakati akichezea Simba SC. 
    CAF iliwabamba kwa urahisi Tanzania, kwa sababu mwaka uliotangulia, Nurdin alisajiliwa na Simba SC kwa ajili ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika na umri wa klabu na shirikisho havikuoana.

    Leodegar Chilla Tenga alikuwa anaanza awamu yake ya kwanza ya Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Makamu wake wa kwanza, Crescentius John Magori wa pili, Alhaj Ismail Aden Rage.
    Vijana wa Tanzania chini ya makocha Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Msaidizi wake, Sylvester Marsh walizitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe ili kupata nafasi hiyo.
    Bahati mbaya kwao, kosa dogo tu la TFF ya Tenga, Magori na Rage liliwakosesha haki yao ya kucheza Fainali za Afrika.
    Vijana hao wa wakati huo ambao sasa wanaitwa wazee, akina Athumani Iddi ‘Chuji’, Omar Matuta ‘Wanchope’, Nizar Khalfan, Amir Maftah, Juma Jabu na wengineo, walisononeka sana kupoteza nafasi hiyo.
    Walisononeka kwa sababu walishiriki michuano hiyo kwa tabu wakitegemea michango ya Watanzania ili kupata fedha za kambi, safari, lishe na huduma zao nyingine zote kwa ujumla.
    Shukrani za dhati ziwaendee IPP Media Limited ambao kupitia vyombo vyao vya habari vya kizalendo, ITV na Radio One waliongoza harambee ya kuhamasisha Watanzania kuichangia Serengeti Boys.
    Siwezi kuisahau sauti nyororo na tamu ya mtangazaji Maulid Baraka Kitenge akiwalilia Watanzania; “Jamani tuisaidieeeni Serengeti Boys”.
    Wenye viroba vya ngano, sembe, sarafu, maharage, dagaa, mbuzi, ng’ombe, kuku, noti na chochote walivukusanya studio za ITV na Radio One pale Mikocheni, Dar es Salaam kabla ya kupelekwa TFF viisaidie Serengeti Boys.
    Unaweza kuona hata Watanzania waliojitolea kuichangia timu yao wakati huo waliumia kiasi gani kwa timu kupokonya tiketi ya kwenda Gambia.
    Imebaki historia- imepita miaka 10 sasa na Tanzania haijaweza kurudia mafanikio hayo licha ya vizazi tofauti kupita kwa kipindi chote hicho.
    Katika kuhakikisha Tanzania inarejesha mafanikio ya Serengeti Boys mwaka 2004, TFF chini ya utawala mpya wa Jamal Emil Malinzi imeomba kuandaa Fainali za vijana U17 mwaka 2019.
    Na ili kuhakikisha wanakuwa na timu imara kushiriki michuano hiyo wakati ukifika, TFF imeanzisha mfuko maalum wa kusaidia maandalizi ya timu hiyo, ambao utakuwa chini ya rais wa zamani wa shirikisho hilo, Tenga.
    Mfuko huo utasimamia timu mbili za vijana chini ya umri wa miaka 12 itakayoanza kuandaliwa mara moja kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa 17 mwaka 2019 pamoja na U14 ambayo itawania tiketi ya Fainali za U17 mwaka 2017 nchini Madagascar.
    Baada ya kuundwa kwa timu hizo, U12 watakwenda kujiunga na shule ya Alliance Academy mjini Mwanza na U14 watakwenda shule ya Lord Burden ya Bagamoyo ambako watakuwa wanasoma na kufanya mazoezi kuandaliwa kwa michuano hiyo.
    Lakini tatizo linakuja wapi zitapatikana fedha za mfuko huo- mwaka 2004 ITV na Radio One waliendesha kampeni ya kuchangisha Watanzania, wakati huo shirikisho halina wadhamini wa kutosha.
    Ligi Kuu ina mdhajini mmoja, Vodacom na Taifa Stars haina mdhamini kabisa- lakini leo Taifa Stars inadhaminiwa na TBL, Ligi Kuu pamoja na kuwa na mdhamini Vodacom, imeuza haki za matangazo ya Talevisheni kwa Azam Media Limited.
    TFF ikaona njia bora ni kutoa fedha kidogo katika mafungu mengine kuingiza kwenye mfuko huo wa maendeleo ya vijana, kuliko tena kuanza kuwachangisha wananchi ambao wengi wao wanalia na ugumu wa maisha.
    TFF ikakutana na viongozi wa Bodi ya Ligi, Mwenyekiti Hamad Yahya na Makamu wake, Sheikh Said Muhammad pamoja na Mtendaji wa kuajiriwa, Silas Mwakibinga kujadiliana juu ya mpango wa kukata asilimia tano ya fedha za udhamini wa Ligi Kuu ziingie kwenye mfuko huo.
    Kwa mujibu wa Malinzi, katika kikao, pande hizo mbili zilikubaliana- lakini baadaye akaibuka Dk Damas Daniel Ndumbaro kwenye mabano PhD, akasema ametumwa na klabu apinge juu ya mpango huo.
    Ndumbaro ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Ligi wa kuteuliwa- aliwaandikia barua TFF kupitia kampuni yake ya uwakili, Meleta & Ndumbaro kuwazuia kukata asilimia tano ya fedha za udhamini wa Ligi Kuu kwa sababu ni kinyume cha mikataba ya Vodacom, wadhamini na akatishia kuitisha mkutano Mkuu wa kumng’oa Malinzi madarakani. 
    Sijui, nasema sijui kwa sababu sijui Ndumbaro anachotaka nini hapa. Sifa, umaarufu au kweli anazihurumia klabu? Sijui. 
    TFF iliwaandikia barua Bodi ya Ligi, ambayo yeye akiwa Mjumbe bila shaka alipata nakala. Hakuna kumbukumbu ya nakala ya barua ya Bodi ya Ligi kuijibu TFF kwa hoja, lakini badala yake Ndumbaro ameenda kuukuza mjadala kwenye vyombo vya Habari.
    Suala hili lingeweza kuwa la mawasiliano ya kiofisi baina ya Kamati ya Utendaji ya TFF na Bodi ya Ligi, hadi wakamalizana wenyewe kimya kimya.
    Wahenga wanasema, mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Malinzi ameunda mfuko wa maendeleo ya vijana na kateua watu wa kuusimamia, tunaowafahamu vyema. 
    Na sababu ya kuunda mfuko huo ni nzuri tu, lengo ni kutafuta sehemu ya kuiinulia soka yetu- lakini anatokea mtu anavalia ‘kibwebwe’ kabisa kupinga.
    TFF si mali ya Malinzi. Ni mali ya Watanzania, leo yupo, kesho ataingia mwingine- lakini wote kwa wajibu mmoja tu, kuongoza soka ya nchi hii.
    Kama tutajengena chuki kiasi cha kupambana hata kupinga masuala ya kimaendeleo kwa ajili ya mpira wa miguu wa nchi yetu wenyewe- tutakuwa wehu.
    Nasema wehu, kwa sababu kama wote tunajenga nyumba moja, kwa nini tuache jukumu la kutumia fito kwa ujenzi wa nyumba yetu na kuanza kuchapana wenyewe? Inasikitisha. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NAMNA HII, TUNAWEZA KUONEKANA WEHU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top