• HABARI MPYA

    Saturday, October 18, 2014

    KIPA ‘PASUA KICHWA’ SIMBA SC IKIMENYANA NA WATANI WAO YANGA SC TAIFA LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MACHO na masikio ya mashabiki wa soka Tanzania, leo vitaelekezwa kwenye mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Miamba hiyo ya soka ya Tanzania, inakutana jioni ya leo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, zikiwa katika taswira mbili tofauti.
    Wakati Ligi Kuu ilianza mwishoni mwa Septemba, mwaka huu, tayari Yang SC imevuna ponti sita kutokana na kushinda mechi mbili na kufungwa moja, wakati mahasimu wao, wameambulia pointi tatu za sare za mechi zao zote.
    Hali hiyo inawafanya mashabiki wa Yanga SC wajiamini timu yao ni bora na wanaingia kwenye mchezo wa leo kwa matumaini makubwa- wakati kwa mahasimu wao, tayari kuna hali ya unyonge.
    Ivo Mapunda amerejeshwa uwanjani mapema licha ya kuwa majeruhi kwa ajili ya mechi na Yanga SC

    Unyonge kwa wana Simba hauletwi tu na matokeo tu, bali hata hali halisi katika kambi ya timu yao, makipa wake wawili wa kwanza, Ivo Mapunda na Hussein Sharrif ‘Cassilas’ wakiwa majeruhi na mlinda mlango pekee aliye fiti, Peter Manyika hajawahi kudaka mechi ya Ligi.
    Mapunda aliumia kidole wiki ya mwisho ya Septemba na akatakiwa kuwa nje kwa wiki nane, lakini kufuatia Cassilas kuumia ugoko kambini Afrika Kusini, Ivo alipandishwa ndege kwenda Johannesburg Jumatatu wiki hii.
    Baada ya kufika Afrika Kusini, Ivo kwanza alifanyiwa vipimo na baadaye akaongezewa tiba ili awe fiti tayari kudaka Jumamosi ya leo.
    Lakini wana Simba SC hawaamini kama Ivo atakuwa tayari kudaka leo na wakati huo huo hawaamini kama ‘dogo’ Manyika anaweza kuhimili vishindo vya pambabo la watani.
    Ukiondoa hilo, wana Simba wana imani na timu yao licha ya sare ya tatu za mwanzo katika Ligi Kuu na wanaamini wanaweza kuifunga Yanga SC.
    Bado imekuwa siri kwa uongozi wa Simba SC juu ya kipa gani atadaka leo kati ya Ivo na Manyika- lakini wazi wote watashiriki mchezo huo, mmoja akianzia benchi.  
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo ni kati ya Polisi Morogoro na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Ndanda FC na Ruvu Shooting Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Kagera Sugar na Stand United Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Coastal Union na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Mbeya City na Azam FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
    Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mchezo kati ya Prisons na JKT Ruvu Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPA ‘PASUA KICHWA’ SIMBA SC IKIMENYANA NA WATANI WAO YANGA SC TAIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top