• HABARI MPYA

    Monday, October 06, 2014

    AYA 15 ZA SAIDI MDOE: MAMA YANGU BI HUSNA HEMED NA WASANII WA BONGO

    JUZI Jumamosi tulimhifadhi mama yetu Bi Husna Hemed (mama yangu mdogo) kwenye makazi yake ya milele pale makaburi ya kisutu jijini Dar es Salaam - Alifariki Ijumaa katika hospital ya AMI alikolazwa kwa siku mbili tu.
    Mama yangu huyu ana historia ya kipekee kwenye maisha yangu pamoja na ndugu zangu wengine wengi, wengi sana - alikuwa ndiye mlezi wetu mkuu kwa hapa Dar es salaam, nyumba yake ilikuwa ndiyo ngome ya shughuli zetu za kifamilia, si harusi, si misiba …hata mie nilipofunga ndoa basi hakukubali niende hotelini kufanya fungate, nikaa nyumbani kwake kwa siku saba kabla ya mimi na mke wangu kwenda kuanza maisha mapya.
    BI Husna Hemed  alikuwa mpenzi wa kazi za wasanii wa Tanzania, alipenda kazi zao, alifurahia ukaribu wangu na wasanii.

    Mara nyingi nilipokuwa nikimtembelea basi asilimia 70 ya maongezi yetu yalihusu wasanii, ataniuliza swali hili na lile kuhusu wasanii, atakusimulia kuhusu vipindi vingi vya televisheni vinavyohusiana na wasanii na alijua ratiba ya vipindi vyote vya aina hiyo.
    Alikuwa akinipigia simu za pole kila aliposikia msanii fulani kafariki, alifanya hivyo akiamini kuwa wasanii wengi ni marafiki zangu. 
    Lakini alikuwa haishii kunipa pole tu bali pia huniuliza kama nilienda kumzika msanii huyo na kwa bahati nzuri mara nyingi alikutana na jibu la NDIO, alikutana na jibu hilo kwa kuwa nimekuwa nikithamini sana wasanii na hivyo kuwa mstari wa mbele kwenye mazishi yao au ya watu wao wa karibu, nimekuwa nikifanya hivyo hata kabla sijafikiria wazo la kuwa na hii website ya Saluti5.
    Alipendelea kuniambia kuwa nisiache kwenda kwenye misiba ya wasanii kwa vile hao ndio watu wangu wa karibu na ndio watakuwa wa kwanza kunifuata pale nitakapokuwa na matatizo, nilitabasamu nikijua wazi hawafahamu vizuri wasanii.
    Nimekuwa nikipoteza karibu siku nzima kwaajili ya kukaa kwenye misiba ya wasanii haswa wale wa dansi na taarab, nimekuwa nikiwafuata bila kujali umbali, wakati hata nje ya Dar es Salaam, sijawahi kuangalia ni namna gani wao wanawajibika kwangu na sijui lini nitaanza kufikiria kufanya hiyo ingawa nadhani upo umuhimu wa kufanya hivyo.
    Kwa kuwa misiba mingi iliyotuhusu ilikuwa ikifanyikia nyumbani kwake (Kinondoni Block 41), basi alikuwa akibahatika kuwaona wasanii kadhaa walionifuta kunifariji, akazidi kupata moyo kuwa wasanii ni watu wangu wa karibu, akapata imani hiyo bila hata kujali kuwa mara nyingi sura alizoziona zilikuwa zile zile.
    “Said  nimeambiwa Mzee Yussuf, Muumin na Chocky wamekuja kuzika, Isha Mashauzi na Asha Baraka pia tulikuwa nao,”  hiyo ni kauli aliyonipa wakati wa msiba wa mama yangu mzazi uliotokea miezi michache iliyopita. Alizoea kunitajia wasanii aliowaona katika kila msiba wetu.
    Siku moja alinichekesha kwa kuaniambia: “Nimeskia Kingwendu alikuwepo, mbona hujamleta ndani anisalimie?” Hakika mama yangu huyu aliwapenda wasanii na aliamini kwenye kila msiba wetu kuna utitiri wa wasanii, sijathubutu hata siku moja kumkatisha tamaa na imani yake hiyo.
    Maskini mama yangu hakujua kama mwanae si pedeshee na hivyo wasanii wengi hawawezi kupoteza muda wao kunifuata – hakujua kuwa kwa vile misiba yetu si ya watu maarufu inayovuta kamera za TV na Blogs, basi wasanii hawawezi kuja kwa wingi kwa vile wengi wao wamejazwa utashi wa kupenda kuuza sura.
    Hakujua kuwa wasanii hata wenyewe kwa wenyewe hawazikani, wanatazama umaarufu wa msiba wa msanii mwenzao, ukiwa huna jina sana basi imekula kwako.
    Huyu ndiye mama yangu aliyewapenda wasanii na kuwaamini wasanii, mama aliyeishi na sisi kwa sehemu kubwa ya umri wetu kuliko tulivyoishi na mama yetu mzazi – mtu ambaye wakati fulani tukageuza nyumba yake kama hoteli, tukawa tukikusanyika kwake na kupata mlo wa usiku, zaidi ya watu 10 tukawa hapo kumtibulia bajeti yake ya chakula kabla ya kuelekea makwetu kulala, maisha yakaendelea hivyo hadi kila mtu alipoa au kuolewa au kwenda kuishi mbali kabisa na Kinondoni – Hakika hakuonyesha kujali. 
    Nichukue fursa hii kuwashukuru wasanii kwa kuja kushiriki mazishi ya mama yetu Bi Husna: Khalid Chokoraa, Mzee Yussuf, Matei Joseph, Siza Mazongela, Isha Mashauzi, Asha Baraka (mmiliki wa Twanga), Omar Baraka (mkurugenzi wa Twanga), Pitshou Mechant, Hamis Dacota (meneja wa Mapacha Watatu, Ismail Suma Raga (meneja wa Mashauzi Classic), Ashraf Mohamed (mkurugenzi wa Melody), Haji Boha (mkurugenzi mipango wa Jahazi), Thabit Abdul, Amin, Ditto, January Eleven, Kalala Jr na wengine ambao pengine kutokana wingi wa watu sikubahatika kuonana nao, nawashukuru sana na nina deni kwenu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AYA 15 ZA SAIDI MDOE: MAMA YANGU BI HUSNA HEMED NA WASANII WA BONGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top