• HABARI MPYA

    Wednesday, October 15, 2014

    7,000 NI NYINGI MNO KWA MLALAHOI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WATANZANIA jana wametimiza miaka 15 tangu wamempoteza baba wa taifa lao, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere- aliyefariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999 mjini London, Uingereza.
    Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, jana vilirejea hotuba na kumbukumbu nyingi juu ya Mwalimu- mwasisi wa taifa na mwanaharakati wa Uhuru wa Tanganyika, ambayo baadaye iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania.
    Moja kati ya hotuba nzuri na za mwishoni za Mwalimu ni ile aliyotoa ukumbi wa Chimwaga, Dodoma wakati wa uchaguzi wa mgombea Urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.


    Benjamin William Mkapa aliteuliwa na CCM na akashinda Urais pia, akiiongoza nchi kwa miaka 10 kabla ya kumuachia Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2005.
    Wakati wa hotuba yake, Mwalimu aliwaambia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kuchagua kiongozi kwa kuzingatia mambo manne, ambayo wakati huo yalikuwa tatizo kwa taifa.
    1. Aliwaambia wachague mgombea ambaye atakuwa anachukia rushwa, 2. Atakayekuwa aanajua Watanzania ni watu masikini, 3 atakayesaidia kupiga vita udini na 4. Atakayesaidia kupiga vita ukabila.
    Mambo hayo hadi leo bado ni kero kwa taifa- rushwa, umasikini, udini na ukabila na maana yake taifa bado linahitaji viongozi ambao watayatambua na kutusaidia kuyatokomeza kabisa.
    Na viongozi wa kusaidia vita hiyo si wa nyanja za kisiasa pekee, bali hata kwenye sekta nyingine mbalimbali, ikiwemo ya michezo. 
    Juzi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetaja viingilio vya mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga utakaofanyika Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kiingilio cha chini kwenye mechi hiyo ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom ni Sh. 7,000 ambacho kitawahusu mashabiki watakaokaa kwenye viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo jumla yake ni 36,693 katika uwanja huo wenye viti 57,558. 
    Viingilio vingine ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
    TFF imesema tiketi zitakazotumika kwenye mechi hiyo ni za elektroniki, na zimeanza kuuzwa mapema wiki hii, zikiwa zinapatikana kwa mtandao wa M-PESA, CRDB Simbanking na maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo zaidi ya mia moja sehemu mbalimbali mjini Dar es Salaam.
    Mechi hiyo namba 27 itakayochezeshwa na mwamuzi Israel Mujuni Nkongo akisaidiwa na John Kanyenye na Ferdinand Chacha itaanza saa 10 kamili jioni. Kamishna wa mechi hiyo ni Salum Kikwamba kutoka mkoani Kilimanjaro.
    TFF chini ya rais wake, Jamal Malinzi imewataka mashabiki kununua tiketi mapema, kwa sababu hazitauzwa uwanjani siku ya mechi. 
    Hakuna tatizo kwa viingilio vya VIP C, B na A, lakini kwa kiingilio cha chini ni kikubwa. Mchezo wa mpira zaidi ni wa watu mafukara, ambao wanajinyima wao na familia zao kwa ajili ya kununua tiketi ya kwenda kuangalia burudani.
    Tathmini inaonyesha nchi za wenzetu Afrika, viingilio vya watu wa chini ni vidogo mno, lakini kwenye maeneo ya VIP ndiyo vinakuwa vikubwa.
    Umefika wakati na TFF iige mfano huo, kwa kuzingatia kwamba Watanzania ni watu masikini. Huyo wa Sh. 30,000 mtoze 100,000, lakini hao unaowatoza 7,000 wafanyie japo Sh. 5,000 ambayo nayo bado ni kubwa vile vile, ispokuwa kwa mechi za Simba na Yanga pekee wanaweza kuhimili. Shlingi 7,000 ni nyingi mno kwa ‘mlalahoi’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: 7,000 NI NYINGI MNO KWA MLALAHOI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top