• HABARI MPYA

  Sunday, May 19, 2019

  SIMBA SC YAIPIGA NDANDA FC NA KUWEKA MKONO MMOJA KWENYE KOMBE LA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Simba SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 2-0 Ndanda FC ya Mtwara katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Ushindi wa leo unawafanya Wekundu hao wa Msimbazi wafikishe pointi 88 katika mchezo wao wa 35 wa msimu na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi tano zaidi ya watani wao wa jadi, Yanga ambao pia wamecheza mechi moja zaidi.
  Sasa Simba SC inatakiwa kushinda mchezo wake wa Jumanne dhidi ya Singida United Uwanja wa Namfua ili kutawazwa rasmi kuwa mabingwa tena wa Ligi Kuu.  Ushindi wa leo wa Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems umetokana na mabao ya mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere mwenye asili ya Rwanda ndani ya robo saa ya kwanza ya mchezo.
  Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC tangu asajiliwe kutoka Gor Mahia ya Kenya, alifunga bao la kwanza dakika ya sita kwa shuti akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, Nahodha, John Raphael Bocco ambaye naye alipokea pasi ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Kagere akamvisha kanzu kipa wa Ndanda FC, Diey Makonga kuifungia bao la pili Simba SC dakika ya 11 na bao lake la 22 la msimu, akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.
  Ndanda wakaamua kucheza kwa kujihami baada ya bao hilo ili kuizuia Simba SC iliyomkosa nyota wake Mganda, Emmanuel Okwi, jambo ambalo liliwasaidia kumaliza mchezo wakiwa wamefungwa ‘2-0 tu’. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aisha Manula, Zana Coulibally, Mohammed Hussein  ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili/Pascal Wawa dk76, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/James Kotei dk46, Haruna Niyonzima, John Bocco/Rashid Juma dk83, Meddie Kagere na Clatous Chama.
  Ndanda FC: Diey Makonga, Aziz Sibo, Yassin Salum, Augustino Nsata,Abdallah Mfuko, Enrick Nkosi, Hassan Maulid, Baraka Majogoro/Emmanuel Memba dk79, Mohammed Mkopi/Yussuf Mhilu dk58, Vitalisy Mayanga na Kiggi Makasi/Salum Chubi dk79.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAIPIGA NDANDA FC NA KUWEKA MKONO MMOJA KWENYE KOMBE LA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top