• HABARI MPYA

    Friday, May 17, 2019

    SAMATTA ATWAA UBINGWA UBELGIJI, KUCHEZA LIGI YA MABINGWA ULAYA MSIMU UJAO

    Na Mwandishi Wetu, BRUSSELS 
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesaidia klabu yake, KRC Genk kutwaa taji la Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji baada ya sare ya 1-1 na wenyeji, Anderlecht usiku wa Alhamisi Uwanja wa Constant Vanden Stock mjini Brussel.
    Kwa sare hiyo, Genk inafikisha pointi 51 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kuelekea mechi za mwisho za msimu, baada ya wapinzani wao wa karibu, Club Brugge kufungwa 2-0 na Standard Liège hivyo kubani na pointi zao 47.
    Katika mchezo wa leo, Genk walitangulia kwa bao la kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen dakika ya 11, kabla ya mshambuliaji Mkongo DR, mzaliwa wa Ufaransa, Yannick Bolasie kuisawazishia Anderlecht dakika ya 65.
    Pamoja na kuipa ubingwa wa Genk, lakini Samatta ambaye leo alipumzishwa dakika ya 76 nafasi yake ikichukuliwa na kiungo Mbelgiji, Casper De Norre, pia anaiwezesha timu yake kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
    Na baada ya mchezo huo, kikosi cha Genk kimerejea nyumbani mjini Genk kwa furaha ambako kesho kutakuwa na sherehe za ubingwa.
    Samatta pia amefanikiwa kuwa ufungaji bora wa Jupiler Pro League kwa mabao yake 23 msimu huu, yakiwemo matatu ya kwenye Championship Round. 
    Kwa ujumla, Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameifungia Genk mabao 62 katika mechi 155 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 katika mechi 122, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA ATWAA UBINGWA UBELGIJI, KUCHEZA LIGI YA MABINGWA ULAYA MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top