• HABARI MPYA

  Wednesday, May 22, 2019

  MO DEWJI KUIPELEKA SIMBA SC KAMBINI MAREKANI, AU URENO KUJIANDAA NA MSIMU UJAO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Bodi ya Simba SC, Mohammed ‘Mo’ Dewji amesema Simba SC itakwenda kuweka kambi Ureno au Marekani kujiandaa na msimu ujao ili iendeleze rekodi yake ya kufanya vizuri.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Dewji pamoja na kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, pia ameelezea mikakati ya msimu ujao.
  “Tunaanza kupanga maandalizi ya msimu, mimi binafsi naongea na timu za Ulaya na Marekani... kuna rafiki yangu anamiliki DC United (Marekani) nimeongea naye watualike tukafanye maandalizi Marekani, kuna uwezekano wa kwenda Ureno, kwenye wiki mbili zijazo tutajua timu itakwenda wapi,” amesema Mo Dewji.

  Mohammed ‘Mo’ Dewji ataipeleka Simba SC Ureno au Marekani kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao 

  Dewji amewapongeza wachezaji kwa kutwaa taji la Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo, kufuatia ushindi wa 2-0 jana dhidi ya Singida United Uwanja wa Namfua.
  "Niwapongeza na kuwashukuru wachezaji wamejitolea kwa namna moja au nyingine hadi tunaupata huu ubingwa, niwashukuru wanachama na wapenzi wote wa Simba kwa kujitokeza kutushangilia. Kocha ameshafikia malengo tuliyomuwekea, tulikuwa tunataka ubingwa na kufika kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa, Mungu akitujalia kwenye wiki moja tutakaa naye tumuongeze mkataba, tutamueleza sehemu ambazo kuna mapungufu ili aendelee kufanyia kazi,”amesema Dewji.
  Aidha, Dewji ameongeza; “Simba itakuwa kwenye soko kushindinda na Al Ahly, Zamalek, TP Mazembe kushindana kutafuta wachezaji wenye vipaji, tupo tayari kuwabakisha wachezaji ambao mwalimu atapendekeza, wengine watatoka kwa mkopo, bajeti ya mwaka huu itakuwa kubwa kuliko mwaka jana,”.
  Kuelekea mchezo wa kesho wa kirafiki dhidi ya Sevilla ya Hispania, Dewji amewashukuru wadhamini wa klabu, SportPesa akisema hii ni mara ya kwanza kwa timu kutoka Ligi Kuu ya Hispania kuja kucheza Tanzania.
  “Ni historia kubwa kwa nchi yetu, tupo tayari kucheza na Sevilla, naomba mashabiki tujitokeze kwa wingi sana. Katika mechi ya kesho ya Sevilla nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili na sisi tuweze kuwaonyesha mpira wa Ulaya,”amesema.
  Baada ya ushindi wa jana, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems imefikisha pointi 91 katika mchezo wa 36 ikijihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu, kwani hakuna timu inayoweza tena kuwafikia. 
  Hilo linkuwa taji la pili mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu kwa Simba SC na la 20 jumla kihistoria baada ya awali kulibeba katika miaka ya 1965, 1966, 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007, 2010, 2012 na 2018.
  Watani wao, Yanga SC ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa Ligi Kuu, mara 27 wakiwa wamebeba taji hilo miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.
  Timu nyingine zilizowahi kubeba taji hilo ni Cosmopolitan 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar mara mbili 1999 na 2000 na Azam FC 2014.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MO DEWJI KUIPELEKA SIMBA SC KAMBINI MAREKANI, AU URENO KUJIANDAA NA MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top