• HABARI MPYA

  Sunday, May 12, 2019

  COASTAL UNION WALIOPIGWA NANE NA SIMBA LEO WAMEIPIGA MTIBWA 1-0 MKWAKWANI

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  TIMU ya Coastal Union leo imeutumia vyema Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Ushindi huo uliotokana na bao pekee la mshambuliaji wake chipukizi, Ayoub Lyanga dfakika ya 74, unafuta machungu ya kichapo cha 8-1 walichopewa na mabingwa watetezi, Simba SC katikati ya wiki Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Coastal Union inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Juma Mgunda inafikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 35 na kujiinua hadi nafasi ya tisa kutoka ya 15.
  Nayo Mtibwa Sugar inayofundishwa pia na mchezaji wake wa zamani, Zubery Katwila inabaki na pointi zake 49 baada ya kucheza mechi 35 pia, sasa ikishika nafasi ya nne. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbeya City imeibuka na ushindi wa ugenini wa 3-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
    
  Mabao ya Mbeya City inayofundishwa na kocha Mrundi, Ramadhani Nswanzurimo yamefungwa na Hamidu Mohamed dakika ya 63, Frank Ikobela dakika ya 81 na Peter Mapunda dakika ya 88. 
  Ushindi huo unaiweka kwenye mazingira salama Mbeya City ikifikisha pointi 43 na kukaa nafasi ya 10 huku Lipuli FC wakibaki nafasi ya tano na pointi 48.
  Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, bao pekee la Baraka Majogoru dakika ya 72 limeipa Ndanda FC ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya African Lyon ambayo tayari imekwishashuka daraja.
  Singida United imelazimishwa sare ya 2-2 na JKT Tanzania Uwanja wa Namfua mjini Singida. Mabao ya Singida yamefungwa na Habib Kiyombo dakika za 30 na 50 na ya JKT yamefungwa na Dickson Chota dakika ya 45 na Samuel Kamuntu dakika ya 78.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: COASTAL UNION WALIOPIGWA NANE NA SIMBA LEO WAMEIPIGA MTIBWA 1-0 MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top