• HABARI MPYA

    Sunday, May 12, 2019

    SAMATTA AKOSA BAO LA WAZI DAKIKA ZA MWISHONI KRC GENK YACHAPWA 3-2 UGENINI

    Na Mwandishi Wetu, BRUGGE
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amekosa bao la wazi dakika za mwishoni, timu yake KRC Genk ikichapwa 3-2 na wenyeji, Club Brugge katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Jan Breydel mjini Brugge.
    Samatta aliunganishwa kwa kichwa krosi kutoka kushoto, mpira ukagonga mwamba na kumrudia akajaribu kupiga tena, lakini beki mmoja wa Club Brugge akaunawa katika harakati za kuokoa, ingawa refa Bram Van Driessche ‘akakausha’.
    Wakati Genk ilikuwa tayari nyuma kwa 3-2, mabao ya Club Brugge yakifungwa na Hans Vanaken dakika ya 53, Lois Openda dakika ya 63 na Krepin Diatta dakika ya 68 wakati ya wageni yalifungwa na Sebastien Dewaest dakika ya nne na Zinho Gano dakika ya 88.
    Mbwana Samatta akisikitika baada ya kukosa bao la wazi wakati huo huo refa akiwanyima penalti
    Mbwana Samatta akiwatoka mabeki wa Club Brugge leo Uwanja wa Jan Breydel mjini Brugge 

    Pamoja na kufungwa, Genk bado inagongoza kwa pointi zake 50 ikifuatiwa na Club Brugge yenye pointi 47 sasa. Genk ilihitaji ushindi leo ili kutangaza ubingwa na sasa italazimika kusubiri kuelekea mechi mbili za mwisho. 
    Hadi sasa, Samatta anaongoza kwenye mbio za ufungaji bora kwa mabao yake 23 msimu huu, yakiwemo matatu ya kwenye Championship Round. 
    Kwa ujumla, Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameifungia Genk mabao 62 katika mechi 154 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 katika mechi 121, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
    Kikosi cha Club Brugge kilikuwa: Horvath, Mata, Mechele, Denswil, Dennis/Poulain dk83, Vormer, Vanaken, Rits/Amrabat dk90+3, Diatta, Writers/Openda dk60 na Wesley.
    KRC Genk: Vukovic, Uronen, Dewaest, Aidoo, Mæhle, Heynen/Gano dk86, Berge, Malinovskyi, Trossard, Ito/Paintsil dk84 na Samatta.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AKOSA BAO LA WAZI DAKIKA ZA MWISHONI KRC GENK YACHAPWA 3-2 UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top