• HABARI MPYA

  Tuesday, May 14, 2019

  ALIYEKUWA KIPA WA SIMBA SC AFAFRIKI DUNIA BAADA YA KUANGUKA MAZOEZINI JESHINI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  ALIYEWAHI kuwa kipa wa Simba SC, kati ya 2012 na 2013, Hamadi Waziri amefariki dunia jana asubuhi baada ya kuanguka mazoezini Uwanja wa Air Winga, Ukonga mjini Dar es Salaam akiwa na timu yake, Transit Camp ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
  Kocha Mkuu wa Transit Camp, Neville Kanza amesema kwamba Waziri amefariki dunia jana baada ya kuanguka mazoezini asubuhi na mwili wake upo hospitali ya Lugalo mjini Dar es Salaam kwa sasa.
  “Hamad tulikuwa naye mazoezini jana Uwanja Air Wing katika hali ya mvua mvua, Uwanja ulikuwa una maji maji na sisi tulikuwa tunafanya mazoezi ya kukimbia, sasa kiatu chake kikafunguka kamba akainama kufunga akainuka na kuanza kukimbia tena, kama hatua mbili hivi akadondoka ghafla kwa kishindo,” amesema Kocha Kanza na kuongeza. 
  “Alidondokea sehemu ngumu ambayo ilimpasua juu ya paji la uso, akakimbizwa hopsitali ya pale pale Air Wing, baada ya kama saa moja madaktari wakathibitisha amefariki ndipo akahamishiwa hospiali ya Lugalo na tunatarajia mwili wake utasafirishwa kesho kwenda kwao Morogoro kwa mazishi,”.
  Hamadi Waziri (kushoto) amefariki dunia jana asubuhi baada ya kuanguka mazoezini Uwanja wa Air Winga, Ukonga mjini Dar es Salaam 

  Hamad alikuwa katika msimu wake wa kwanza tu Transit Camp baada ya kujiunga nayo akitokea JKT Tanzania ambayo nayo ilimtoa timu nyingine ya jeshi, Mlale JKT.
  Ikumbukwe Mlale JKT ilimsajili Waziri baada ya kuachwa na Simba SC ambayo iliyomsajili kutoka Maji Maji ya Songea. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Hamad Waziri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ALIYEKUWA KIPA WA SIMBA SC AFAFRIKI DUNIA BAADA YA KUANGUKA MAZOEZINI JESHINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top