• HABARI MPYA

  Alhamisi, Mei 30, 2019

  RAIS WA FIFA, INFANTINO AIPONGEZA SIMBA SC KWA KUTWAA TENA UBINGWA WA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) Gianni Infantino ametuma salamu za pongezi kwa Klabu ya Simba kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
  Infantino ametuma salamu hizo za pongezi kupitia kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia.
  Katika Salamu hizo Infantino amesema amefurahishwa kusikia Simba SC wamevikwa taji la Ubingwa wa Ligi Kuu 2018/2019 ikiwa ni mara ya pili mfululizo jambo ambalo ni la kupongezwa.
  Amesema hayo ni majibu ya jitihada na juhudi na ameomba salamu hizo zifikishwe kwa uongozi, wachezaji, kocha na benchi lake zima la ufundi, Madaktari pamoja na mashabiki na kuwataka kuendeleza uthubutu na hamasa.

  Rais wa FIFA, Gianni Infantino (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa 

  Infantino kwa niaba ya Jamii ya Mpira Kimataifa ameishukuru Simba na TFF kwa kusaidia kusambaza ujumbe chanya wa Mpira wa Miguu ambao unajumuisha watu wote.
  Akimalizia salamu zake kwa Rais wa TFF,Infantino amesema anatarajia watakutana kwenye Kongamano la 69 la FIFA litakalofanyika Paris.
  Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems imemaliza Ligi Kuu na pointi 93, zikiwa ni saba zaidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC waliomaliza na pointi 86 katika nafasi ya pili, wakati Azam FC imeshika nafasi ya tatu kwa pointi zake 75. 
  Hilo linkuwa taji la pili mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu kwa Simba SC na la 20 jumla kihistoria baada ya awali kulibeba katika miaka ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007, 2010, 2012 na 2018.
  Watani wao, Yanga SC ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa Ligi Kuu, mara 27 wakiwa wamebeba taji hilo miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.
  Timu nyingine zilizowahi kubeba taji hilo ni Cosmopolitan 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar mara mbili 1999 na 2000 na Azam FC 2014.
  Wakati Simba SC ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo, Stand United ya Shinyanga imeungana na African Lyon ya Dar es Salaam kuteremka daraja na – Kagera Sugar ya Bukoba na Mwadui FC ya Shinyanga zitamenyana na timu za Daraja la Kwanza, Pamba SC na Geita Gold kuwania kubaki Ligi Kuu katika mechi za mchujo.
  Mechi za kwanza za mtoano zitapigwa Juni 2, Kagera ikianzia ugenini Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Mwadui ikianzia ugenini dhidi ya Geita kabla ya marudiano Juni 8 Uwanja wa Kaitaba Bukoba na Mwadui Complex, Shinyanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RAIS WA FIFA, INFANTINO AIPONGEZA SIMBA SC KWA KUTWAA TENA UBINGWA WA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top