• HABARI MPYA

    Saturday, May 25, 2019

    SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA BIASHARA UNITED, SASA KOMBE WATAPEWA MORO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ZOEZI la kuikabidhi Simba SC Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara limeshindikana leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam ikilazimishwa sare ya 1-1 na Biashara United.
    Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura amesema leo kwamba imeshindikana SImba SC kukabidhiwa Kombe kutokana na kutokana na kutofika kwa mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye ametoa udhuru.
    Hata hivyo, Wambura amesema kwamba Simba SC watakabidhiwa Kombe lao Jumanne katika mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Waziri Lugola ameahidi kuhudhuria.
    Viungo Haruna Niyonzima wa Simba SC (kulia) na George Makang'a wa Biashara United (kushoto) wakiwania mpira leo Uwanja wa Taifa

    Katika mchezo wa leo, Biashara United inayofundishwa na beki na kocha Msaidizi wa zamani wa Simba SC, Amri Said ‘Stam’ ilitangulia kwa bao la Innocent Edwin dakika ya 14.
    Lakini dakika tatu tu baadaye, kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama akaisawazishia Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems bao hilo dakika ya 17.  
    Kutoka hapo mchezo ukawa ni wa kushambuliana kwa zamu na kosa kosa za pande zote mbili, huku Nahodha wa Simba SC, John Raphael Bocco na kinara wa mabao Ligi Kuu, Mnyarwanda Meddie Kagere wakipoteza nafasi za wazi.
    Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, JKT Tanzania imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa JKM Park, eneo la Gerezani mjini Dar es Salaam.
    Ikumbukwe mchezo huo ni kiporo cha juzi na jana baada ya kushindikana kufanyika kwa sababu ya mvua kuharibu Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni na kulazimika kuhamishiwa JMK Park ambako mabao ya Hassan Matalema dakika ya 26 na 90 yakawapa ushindi wenyeji.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Muzamil Yassin, Clatous Chama, Haruna Niyonzima/Hassan Dilunga dk71, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi. 
    Biashara United; Nourdine Balora, Derrick Mussa, Nassib Mpapi, Lameck Chamkaga, Abdulmajid Mangalo/Kauswa Bernard dk69, Wilfred Nkouluma, Juma Mpakala, Taro Donald, Tariq Seif, Innocent Edwin na George Makang'a.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA BIASHARA UNITED, SASA KOMBE WATAPEWA MORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top