• HABARI MPYA

  Sunday, May 19, 2019

  RAIS WA ZAMANI WA ZFA NA CECAFA ALI FEREJ TAMIM AFARIKI DUNIA LEO ZANZIBAR

  Na Salum Vuai ZANZIBAR
  ALIYEWAHI kuwa Rais wa muda mrefu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA-Sasa ZFF) Ali Ferej Tamim, amefariki dunia leo mjini Zanzibar. 
  Marehemu Ferej aliyeiongoza ZFA kwa zaidi ya miaka 20 tangu, amekutwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mrefu na kulazimika kufanyiwa upasuaji nchini India mapema mwaka jana.
  Katika kipindi cha uongozi wake ZFA, alishiriki kikamilifu katika jitihada za kuiombea Zanzibar uanachama wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) tangu lilipokuwa chini ya urais wa Joao Havellenge.

  Aidha, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na baada ya  kustaafu alikuwa mjumbe wa heshima katika baraza hilo.
  Ferej aliyefariki akiwa na umri wa miaka 67, alizaliwa tarehe 27 Oktoba, 1952 mjini Zanzibar, na aliichezea klabu kongwe ya Malindi SC na baadae kuwa kocha wa timu hiyo kwa miaka kadhaa.
  Akishirikiana na wasaidizi wake, aliisaidia Zanzibar kupata uanachama shirikishi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inaoendelea nao hadi sasa.
  Mazishi ya marehemu Ferej yamefanyika leo katika makaburi ya Mwanakwerekwe nje kidogo ya manispaa ya Mjini Zanzibar, baada ya kusaliwa katika msikiti wa Ijumaa, Malindi. 
  Wakati huo huo: Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kwa Familia,Ndugu, jamaa,marafiki na ZFA kufuatia kifo cha Tamim.
  Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo amesema kwamba marehemu Tamimu kama mmoja wa Wanamichezo waliotoa mchango mkubwa katika Mpira wa Miguu hususani Visiwani Zanzibar.
  “Ni ukweli usiofichika Marehemu Tamimu alikua na mchango mkubwa katika Mpira wa Miguu wa Tanzania hususani Zanzibar ambako amekua kiongozi kwa miaka kadhaa,Kwa niaba ya TFF natoa pole kwa Familia,Ndugu, Jamaa,Marafiki na ZFA ambayo amewahi kushika wadhifa wa juu kabisa” amesema Karia.
  Ameongeza kuwa katika kipindi hiki kigumu TFF inaungana na Wafiwa pamoja na Wanamichezo wote. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu pahala pema Peponi. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS WA ZAMANI WA ZFA NA CECAFA ALI FEREJ TAMIM AFARIKI DUNIA LEO ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top