• HABARI MPYA

  Thursday, May 23, 2019

  GEITA GOLD, PAMBA SC ZAFUZU ‘PLAY-OFF’ KUPANDA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU za Pamba SC ya Mwanza na Geita Gold SC ya Geita, zimefuzu kucheza hatua ya mtoano (play-off) kuwania kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
  Pamba imepata fursa hiyo baada ya kuifunga Mbeya Kwanza mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Dimba la Nyamagana jijini Mwanza na kufuzu kwa goli la ugenini kufuatia kipigo cha mabao 3-1 ilichokipata kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa mkoani Mbeya wiki iliyopita.
  Kwa upande wa Geita Gold, imepata nafasi hiyo baada ya kutoka suluhu ugenini na Mlale JKT kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa mkoani Ruvuma na kufuzu kwa ushindi wa mabao 3-0 ilioupata nyumbani wiki iliyopita.
  Katika mechi za mtoani (play-off) kusaka timu mbili za kushuka na kupanda daraja, Pamba itakutana na timu itakayomaliza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa nafasi ya 18, huku Geita ikisubiri timu itakayomaliza ligi kuu ikiwa nafasi ya 17 na timu zitakazofanya vizuri zibaki au kupanda ligi kuu msimu ujao.
  Tayari timu mbili ambazo ni Namungo FC na Polisi Tanzania zimekwishapanda ligi kuu moja kwa moja baada ya kuongoza kwenye makundi yao huku Pamba na Geita zikilazimika kupitia hatua ya mtoano baada ya kushika nafasi ya pili na ya tatu kwenye makundi yao.
  Katika Ligi Daraja la Kwanza iliyomalizika hivi karibuni, kinara wa Kundi A alikuwa ni Namungo FC akifuatiwa na Mbeya Kwanza pamoja na Mlale JKT wakati kinara wa kundi B akiwa ni Polisi Tanzania akifuatiwa na Pamba SC huku Geita ikimaliza nafasi ya tatu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GEITA GOLD, PAMBA SC ZAFUZU ‘PLAY-OFF’ KUPANDA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top