• HABARI MPYA

  Thursday, May 30, 2019

  ADI YUSSUF AWA MCHEZAJI WA KWANZA KUSAJILIWA BLACKPOOL YA LIGUE 1 ENGLAND

  Na Mwandishi Wetu, LANCASHIRE 
  MSHAMBULIAJi chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Adi Yussuf amekuwa mchezaji wa kwanza kabisa dirisha hili kusajiliwa na timu ya Blackpool FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili England ijulikanayo kama Ligue 1.
  Yussuf mzaliwa wa kisiwani Zanzibar, amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya tatu kwa ukubwa England baada ya Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, huku kukiwa na kipengele cha kuongezewa mwaka mmoja akifanya vizuri.
  Yussuf mwenye umri wa miaka 27 sasa, anajiunga na Blackpool yenye maskani yake Lancashire akitokea Solihull Moors kama mchezaji huru.
  Adi Yussuf amekuwa mchezaji wa kwanza dirisha hili kusajiliwa na Blackpool FC ya Ligue 1 England

  Baada ya kufunga mabao 21 katika mashindano yote Solihull Moors, yakiwemo mawili dhidi ya Seasiders kwenye mchezo wa marudiano wa Raundi ya Pili ya Kombe la FA na kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye National League, Yussuf ameamua kwenda kujaribu changamoto mpya kwenye soka.
  Yussuf ni miongoni mwa wachezaji 39 walioitwa kwenye kikosi cha awali cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwezi ujao nchini Misri.
  Mchezaji huyo wa zamani wa akademi ya Leicester City, rekodi yake nzuri zaidi ya msimu ni kufunga mabao 29 katika mechi 39 akiwa na Oxford City msimu wa 2014- 2015 baada ya awali kuchezea Burton Albion, Mansfield Town na Crawley Town.
  Akizungumza baada ya kukamilisha usajili wake huo, Adi Yussuf alisema; “Ndoto zimetimia kwangu. Kazi ngumu, kujitolea kwangu na kujituma msimu huu vimelipa. Natoa shukrani zangu za dhati kwa kila mmoja aliyechangia mafganikio yangu na kila mtu Solihull. Nina uhakika ninaweza kucheza ligi kuu,” amesema.
  Naye kocha wa Blackpool, Terry McPhillips amesema kwamba ana matumaini makubwa na Adi, kwani amekuwa akimfuatilia kwa muda mrefu na amejiridhisha na uwezo wake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ADI YUSSUF AWA MCHEZAJI WA KWANZA KUSAJILIWA BLACKPOOL YA LIGUE 1 ENGLAND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top