• HABARI MPYA

  Tuesday, May 14, 2019

  YANGA SC YAREJEA KILELENI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA RUVU SHOOTING 1-0 LEO UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 83 baada ya kucheza mechi 36, sasa ikiwazidi pointi moja, mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi tatu mkononi.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hussein Athuman wa Katavi aliyesaidiwa na John Kanyenye wa Mbeya na Agness Pantaleo Arusha, bao pekee la Yanga SC lilifungwa na kiungo Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

  Tshishimbi alifunga bao hilo dakika ya 15 akimalizia pasi ya Deus David Kaseke alipokea pasi ya kichwa ya Raphael Daudi Lothi, wote viungo kufuatia majaro iliyoingizwa na beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali.
  Kipindi cha pili timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini Yanga SC ikafanikiwa kulinda bao lake na kubeba pointi tatu za mchezo huo.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Mwaduo FC imelazimishwa sare ya 3-3 na jirani zao, Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.
  Mabao ya Mwadui FC yamefungwa na Ottu Joseph mawili, dakika za 46 na 69 na Gerald Mathias dakika ya 58, wakati ya Mbao FC yamefungwa na Abubakar Ngalema dakika ya 35, Said Junior dakika ya 44 na Hamim Abdul dakika ya 86. 
  Kikosi cha Ruvu Shooting kilikuwa; Abdallah Rashid, George Amani, Edward Manyama, Santos Mazengo, Tumba Sued/Damas Makwaya dk83, Zuberi Dabi/Khamis Mcha dk48, William Patrick, Shaaban Msala, Fully Zully Maganga, Baraka Mtuwi na Emmanuel Martine.
  Yanga SC; Klaus Kindoki, Juma Abdul/Ibrahim Ajib dk57, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Paul Godfrey, Raphael Daudi/Thabani Kamusoko dk66, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na Deus Kaseke/Said Juma ‘Makapu’ dk82.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAREJEA KILELENI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA RUVU SHOOTING 1-0 LEO UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top