• HABARI MPYA

  Thursday, May 30, 2019

  KAGERE AWA MCHEZAJI BORA WA MWAKA SIMBA SC, OKWI ATOKA MIKONO MITUPU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere ameibuka kinara katika tuzo za Mo Simba kwa kushinda tuzo mbili – Mchezaji Bora na Mfungaji Bora wa Mwaka katika usiku ambap nyota Mganda, Emmanuel Okwi ametoka mikono mitupu.
  Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC tangu ajiunge nayo kutoka Gor Mahia ya Kenya katika tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka amewashinda Nahodha na mshambuliaji mwenzake, John Raphael Bocco na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
  Tuzo ya ufungaji bora amepewa moja kwa moja kwa kuwa mfungaji bora wa msimu wa klabu na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara akiiwezesha na timu yake kutwaa taji hilo. 
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere ndiye Mchezaji Bora wa Mwaka Simba SC 

  Beki anayeweza kucheza nafasi za kiungo pia, Erasto Edward Nyoni naye pia amepata tuzo mbili, Mchezaji Bora wa Wachezaji na Beki Bora wa Mwaka. Katika tuzo ya Beki Bora amewashinda Muivory Coast Serge Wawa Pascal na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Tanzania, Shomary Kapombe.
  Kipa bora ni Aishi Manula aliyemshinda Deogratius Munishi ‘Dida’, kiungo Bora ni Mghana James Kotei aliyewashinda Jonas Mkude na Muzamil Yassin, wakati Mshambuliaji Bora ni Nahodha, Bocco aliyewashinda Kagere na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi.
  Chama amejishindia tuzo ya Goli Bora kwa bao lake zuri alilofunga kwenye mechi ya hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana FC ya kwao, Zambia. Bao lake hilo limelizidi lile alilofunga dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwebnye hatua ya makundi.
  Na amewashinda Kagere aliyeingia na bao pekee alilofunga katika ushindi wa 1-0 dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga na Bocco aliyeingia na bao alilofunga dhidi ya Biashara United ya Mara.
  Rashid Juma ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka, Mwanahamisi Omary Shaluwa ‘Gaucho’ ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Mwanamke wa Mwaka na mfadhili wa zamani wa klabun hiyo, Azim Dewji ameshinda Tuzo ya Heshima baada ya kuiwezesha klabu kufika fainali ya Kombe la CAF 1993.
  Tuzo za Mo Simba zinafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo tangu zianzishwe na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohammed Dewji. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERE AWA MCHEZAJI BORA WA MWAKA SIMBA SC, OKWI ATOKA MIKONO MITUPU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top