• HABARI MPYA

  Friday, May 17, 2019

  MAKAMBO ‘KWAHERI YANGA SC’, ASAINI MKATABA WA KUJIUNGA NA HOROYA AC YA GUINEA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Heritier Ebenezer Makambo amekamilisha mwaka wake mmoja wa kuitumikia klabu ya Yanga ya Dar es Salaam kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Horoya AC ya Guinea.
  Makambo aliwasili mjini Conakry Jumatano akiwa ameongozana na kocha wa Yanga, Mkongo mwenzake, Mwinyi Zahera na Alhamisi akasaini mkataba huo.
  Mwenyekiti mpya wa klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msolla amethibitisha Zahera kwenda na Makambo Guinea kwa mazungumzo na Horoya Athletic Club na baada ya hapo wataleta ofa ya kumnunua.

  Heritier Makambo amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Horoya AC ya Guinea 

  “Makambo aliondoka na mwalimu (Zahera) ili akamsimamie, mambo yakienda sawa sawa kwa sababu uwezo wake wamekwishauona wataleta barua rasmi sasa kuonyesha ofa ambayo wanaipa klabu,”amesema Dk. Msolla na kufafanua kuhusu kuvuja kwa picha mchezaji huyo akisaini;
  “Tumeona hizo picha na sisi kwenye mtandao, tunamngojea mwalimu arudi kesho atautaarifu uongozi kilichotokea kule na mazungumzo yamekwendaje, sisi tutakachongojea ni taratibu za mpira, sheria zinasemaje, tunangojea ofa na kama itakuwa inavutia, tutamruhusu”.
  Msolla, kocha wa zamani wa Taifa Stars amesema kwamba wachezaji wote, wazawa na wageni ajira yao ni soka hivyo wanavyopata nafasi kwenda kucheza kwenye maslahi mazuri zaidi, vyema kuwaruhusu ili pia klabu ipate nafasi ya kusajili nyota wengine. 

  Horoya Athletic Club, inayofahamika pia kama Horoya Conakry au H.A.C. ni klabu kongwe Guinea yenye maskani yake mjini Conakry, ambayo ilianzishwa mwaka 1975.
  Na Makambo anaondoka Yanga akiwa kinara wa mabao wa timu hiyo, hadi sasa akiwa ameifungia mabao 16 kwenye Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAKAMBO ‘KWAHERI YANGA SC’, ASAINI MKATABA WA KUJIUNGA NA HOROYA AC YA GUINEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top