• HABARI MPYA

  Thursday, May 16, 2019

  ALLIANCE YAIWEKA PABAYA BIASHARA UNITED, MBEYA CITY YAIUA COASTAL DAKIKA YA MWISHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Alliance FC ya Mwanza jana imewaadhibu wapinzani wao wa Kanda ya Ziwa, Biashara United kwa kuwachapa 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
  Mabao ya Alliance FC yalifungwa na mkongwe, mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC ya dar es Salaam na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Javu dakika ya saba na Mnigeria Michael Chinedu dakika ya 71, wakati la Biashara United limefungwa na Tariq Kiakala dakika ya 22.
  Kwa ushindi huo, Alliance FC inafikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 36 na kujiinua kutoka nafasi ya 15 hadi ya 10, wakati Biashara United inayobaki na pointi zake 40 baada ya kucheza mechi 35 inabaki nafasi ya 18 kwenye ligi ya timu 20. 

  Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu jana, bao pekee la Iddi Suleiman ‘Naldo’ dakika ya 90 na ushei liliipa ushindi wa 1-0 Mbeya City dhidi ya Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Kwa matokeo hayo, Mbeya City inafikisha pointi 46 katika mchezo wa 35 na kupanda hadi nafasi ya nane kutoka ya 11, wakati Coastal Union inayobaki na pointi zake 44 baada ya kucheza mechi 36 inabaki nafasi ya tisa.
  Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea leo kwa mabingwa watetezi, Simba SC kuwakaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ALLIANCE YAIWEKA PABAYA BIASHARA UNITED, MBEYA CITY YAIUA COASTAL DAKIKA YA MWISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top