• HABARI MPYA

  Friday, May 10, 2019

  AZAM FC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA KMC CHAMAZI, AFRICAN LYON YATEREMKA TENA DARAJA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imelazimishwa sare ya bila kufungana nan a KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Sare hiyo inayoiongezea kila timu pointi moja, inaifanya Azam FC ifikishe pointi 68 baada ya kucheza mechi 35 ingawa inabaki nafasi ya tatu, wakati KMC inafikisha pointi 46 katika mchezo wa 35 pia, nayo ikibaki nafasi ya sita.
  Simba SC ndiyo inayoongoza Ligi Kuu kwa sasa, ikiwa na pointi 81 baada ya kucheza mechi 31, ikiwazidi pointi moja watani wao wa jadi, Yanga ambao hata hivyo wamecheza mechi tatu zaidi.

  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, African Lyon imechapwa mabao 3-2 na Mbao FC Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanaifuta kabisa Lyon kwenye orodha ya timu za Ligi Kuu msimu ujao, ikibaki na pointi zake 22 baada ya kucheza mechi 34, huku Mbao FC ikifikisha pointi 43 katika mchezo wa 35 na kujiinua hadi nafasi ya 10 kutoka ya 14.
  Nayo Ruvu Shooting ikaichapa 2-0 Lipuli FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, mabao ya Emmanuel Martin dakika ya 35 na William Patrick dakika ya 38.
  Stand United imelazimishwa sare ya 2-2 na Singida United Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Mabao ya Stand United yamefungwa na Hafidh Mussa dakika ya 37 na Jacob Masawe dakika ya 59, wakati ya Singida United yamefungwa na Boniphace Maganga dakika ya 44 na Habibu Kyombo dakika ya 55.
  Singida United sasa ni ya saba ikiwa na pointi 44 za mechi 35, Ruvu Shooting ya 11 kwa pointi zake 42 za mechi 35 na Stand United sasa ni ya 13 ikiwa na pointi 41 za mechi 35.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA KMC CHAMAZI, AFRICAN LYON YATEREMKA TENA DARAJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top