• HABARI MPYA

    Friday, February 01, 2019

    SIMBA YASAJILI MSHAMBULIAJI WA NDANDA, COULIBALY RUKSA KUWAVAA AHLY KESHO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI chipukizi wa Ndanda FC ya Mtwara, Vitalis Mayanga amejiunga rasmi na klabu Simba SC ya Dar es Salaam.
    Mayanga anajiunga na Simba SC katika dirisha dogo la usajili la Januari baada ya kuitumikia timu ya Mtwara kwa nusu msimu tu kufuatia kujiunga na nayo kutoka Stand United ya Shinyanga.
    Mayanga ni kati ya wachezaji waliokuwapo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 kilichotolewa na Burundi katika mechi za kufuzu Olimpiki ya mwakani Japan.

    Vitalis Mayanga (kulia) akiichezea Stand United dhidi ya Simba SC msimu uliopita Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. Kushoto ni Muzamil Yassin 

    Pamoja na Mayanga, Simba SC imefanikiwa kupata leseni ya beki wake mpya, Zana Coulibaly kutoka Burkina Faso kwa ajili ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Kwa kupewa leseni hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Coulibaly sasa anaweza kuanza kuitumikia Simba SC kesho katika mechi za Kundi D Ligi ya Mabingwa. 
    Simba SC watakuwa wageni wa Al Ahly kuanzia Saa 4:00 kesho Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria, Misri katika mchezo utakaochezeshwa na marefa kutoka Senegal.
    Hao ni Maguette Ndiaye atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera Djibril Camara na El Hadji Malick Samba wakati mezani atakuwepo  Daouda Gueye.  
    Simba inashika nafasi ya tatu katika Kundi D ikiwa na pointi tatu sawa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inayoshika nafasi ya pili kwa wastani wake nzuri wa mabao, wakati Ahly inaongoza kwa pointi zake nne na JS Saoura ya Algeria inashika mkia kwa pointi yao moja. 
    Baada ya ushindi wa 3-0 nyumbani na kipigo cha 5-0 kutoka Vita mjini Kinshasa katika mechi zake mbili za kwanza za Kundi D, Simba SC imepania kupigana kiume kupata matokeo mazuri kesho Alexandria.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YASAJILI MSHAMBULIAJI WA NDANDA, COULIBALY RUKSA KUWAVAA AHLY KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top