• HABARI MPYA

    Friday, December 14, 2018

    HARUNA MOSHI ‘BOBAN’ ASAINI MKATABA WA MIEZI SITA KUJIUNGA NA YANGA SC, KOCHA MWINYI ZAHERA ASEMA…

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO mshambuliaji mkongwe, Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ amesaini mkataba wa miezi sita kujiunga na klabu ya Yanga akitokea African Lyon, zote za Dar es Salaam.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya klabu ya Yanga, Hussein Nyika amemtambulisha Boban Alhamisi kuwa mchezaji mpya na wa kwanza rasmi kusajiliwa katika dirisha hili dogo.
    Yanga SC pia ipo mbioni kumsajili winga Ruben Bomba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye tayari yupo nchini kwa wiki tatu sasa.
    Kocha Mkongo wa Yanga SC, Mwinyi Zahera amesema kwamba yeye ndiye amependekeza Boban asajiliwe baada ya kumuona akicheza vizuri na klabu ya African Lyon. 
    Haruna Moshi 'Boban' (kushoto) akisaini mkataba wa kujiunga na Yanga leo. Kulia ni Hussein Nyika, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga

    Haruna aliyepewa jina la utani Boban kutokana na kufananishwa kiuchezaji na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Croatia na AC Milan, Zvonimir Boban ambaye kwa sasa ni Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), alizaliwa mwaka 1987 mjini Tabora, yaani anazidiwa na wote, Mnyarwanda Meddie Kagere na Muivory Coast, Serge Wawa Pascal wa Simba SC waliozaliwa mwaka 1986.
    Kisoka aliibukia Tabora kabla ya kujiunga na sekondari ya vipaji maalum vya wanamichezo, Makongo mjini Dar es Salaam mwaka 2001 na mwaka 2002 akasajiliwa kwa mara ya kwanza na klabu ya Ligi Kuu, Coastal Union ya Tanga akiwa ana umri wa miaka 15 tu.
    Alidumu kwa msimu mmoja huko kabla ya kujiunga na Moro United mwaka 2003 alikocheza hadi 2004 alipohamia Simba SC ambako alicheza hadi mwaka 2010 alipouzwa Gefle IF ya Ligi Kuu ya Sweden.
    Hata hivyo, katika mastaajabu ya wengi, pamoja na kukubalika Ulaya, Boban alirejea nyumbani Tanzania mwaka 2011 na kusiani tena Simba SC.
    Baadaye alikwenda Oman kujiunga na Muscat Club kabka ya kurejea tena SImba SC ambako mwaka 2012 aliachwa kwa kile kilichoelezwa utovu wa nidhamu naye akaenda kujiunga na Coastal Union ya Tanga.
    Alicheza Coastal Union kwa msimu mmoja kabla ya kuhamia Mbeya City ambako nako pia hakudumu akarejea Dar es Salaam kuchezea timu ya Daraja la Kwanza, Friends Rangers kabla ya msimu huu kujiunga na African Lyon aliyoichezea katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu hadi kumvutia kocha Mkongo wa Yanga, Mwinyi Zahera.
    Boban amekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu mwaka 2004 ingawa kwa vipindi tofauti amekuwa akiachwa kwa sababu za utovu wa nidhamu na tangu mwaka 2009 baada ya Fainali za CHAN nchini Ivory Coast hakuwahi kuitwa tena Taifa Stars.
    Ni kipenzi cha mashabiki wengi wa soka nchini akitukuzwa kama mmoja wa wachezaji wenye vipaji vya kipekee, ingawa wakati wote tuhuma za utovu wa nidhamu zimekuwa zikimuwekea mazingira magumu ya kikazi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HARUNA MOSHI ‘BOBAN’ ASAINI MKATABA WA MIEZI SITA KUJIUNGA NA YANGA SC, KOCHA MWINYI ZAHERA ASEMA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top