• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 27, 2018

  SAMATTA AENDELEZA MOTO WA MABAO GENK IKISHINDA 3-1 LIGI YA UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana ameendeleza makali yake ya kufunga, timu yake, KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya AA Gent katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Samatta jana alifunga bao la kwanza katika ushindi huo dakika ya 23, ambalo lilikuwa ni la kusawazisha baada ya Mwafrika mwenzake, beki Mtunisia Dylan Bronn kutangulia kuwafungia wageni dakika ya sita.
  Mabao mengine ya Genk yalifungwa na Wabelgiji, beki Sebastien Dewaest dakika ya 47 na kiungo Bryan Heynen dakika ya 85.

  Ushindi huo unazidi kustawisha uongozi wa Genk katika Ligi Kuu ya Ubelgiji, sasa ikifikisha pointi 48 baada ya kucheza mechi 21, ikiwazidi kwa pointi 10, Club Brugge wanaofuatia nafasi ya pili, ingawa wamecheza mechi 20.
  Samatta mwenye umri wa miaka 26, amefikisha jumla ya mabao 54 katika mechi 137 za mashindano yote alizoichezea KRC Genk tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kwenye Ligi ya Ubelgiji amefikisha mabao 39 katika mechi 105, wakati Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 22 na katika Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa.
  Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa: Vukovic, Maehle, Aidoo, Dewaest, Uronen, Berge, Heynen, Pozuelo, Ndongala/Gano dk89, Paintsil/Zhegrova dk90+2 na Samatta.
  AA Gent; Thoelen, Souquet, Rosted, Odjidja/Verstraete dk67, Diarra, David/Awoniyi dk74, Yaremchuk, Dejaegere, Asare, Bronn/Plastun dk58 na Esiti.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AENDELEZA MOTO WA MABAO GENK IKISHINDA 3-1 LIGI YA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top