• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 29, 2018

  KICHUYA AFUNGA MAWILI SIMBA SC YAISHINDILIA SINGIDA UNITED 3-0 TAIFA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeonyesha bado imo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida United jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 33 baada ya kucheza mechi 14, ikiendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 40 za mechi 17 na Yanga SC wenye pointi 50 za mechi 18. 
  Mabao ya Simba SC katika mchezo wa leo yamefungwa na wachezaji wazalendo watupu, mshambuliaji na Nahodha John Raphael Bocco na kiungo Shiza Ramadhani Kichuya aliyefunga mawili.
  Shiza Kichuya akikimbia kushangilia baada ya kufunga bao la kwanza kati ya mawili leo
  Shiza Kichuya akiwatoka wachezaji wa Singida United leo Uwanja wa Taifa 
  Mshambuliaji John Bocco akimtoka beki wa Singida United, Rajab Zahir leo
  Kiungo Mzambia, Clatous Chama akimiliki mpira katikati ya wachezaji wa Singida United
  Kikosi cha Simba SC kilichoanza katika mchezo wa leo
  Kikosi cha Singida United kilichoanza katika mchezo wa leo

  Kichuya alianza kwa kumsetia Bocco kufunga bao la kwanza dakika ya 17 kabla ya yeye mwenyewe kufunga dakika za 49 na 54 mara zote akimalizia pasi maridadi za kiungo Mzambia, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’.
  Singida United ilipata pigo ndani ya nusu saa tu kufuatia kiungo wake Issa Abdi Makamba kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Asad Ali Juma.
  Simba SC iliyomkosa mshambuliaji wake, Mnyarwanda Meddie Kagere ambaye ni majeruhi, ingeweza kuondoka na ushindi mkubwa zaidi kama ingetumia vyema nafasi nyingi ilizotengeneza kwenye mchezo wa leo.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Nicholas Gyan/Zana Coulibaly dk66, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco/Muzamil Yassin dk81, Shiza Kichuya/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk84 na Emmanuel Okwi.
  Singida United: Ally Mustafa ‘Barthez’, Issa Makamba/Asad Juma dk29, Mohammed Abdallah, Salum Kipiga, Kennedy Juma, Rajab Zahir, Boniface Maganga, Yussufu Kagoma, Ike Obina/Geoffrey Mwashiuya dk78, Kenny Ally na Habibu Kiyombo/Frank Mkumbo dk58.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KICHUYA AFUNGA MAWILI SIMBA SC YAISHINDILIA SINGIDA UNITED 3-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top