• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 20, 2018

  SAMATTA AKOSA PENALTI GENK YATUPWA NJE KWA MATUTA KOMBE LA UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amekosa penalti timu yake, KRC Genk ikifungwa kwa penalti 4-3 na Union Saint-Gilloise ya Ligi Daraja la Kwanza B, kufuatia sare ya 2-2 Uwanja wa Joseph Marien mjini Brussells katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Ubelgiji.
  Kwa matokeo hayo, safari ya Genk inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza A Ubelgiji, katika Kombe la Ligi ya Ubelgiji inafikia Robo Fainali, huku Union Saint-Gilloise inayoshiriki ligi ya pili kwa ukubwa nchini humo ikiungana na Gent, Mechelen na KV Oostende kwenda Nusu Fainali.
  Katika mchezo wa jana, Samatta aliingizwa dakika ya 114 kwenda kuchukua nafasi ya Msenegali, Ibrahima Seck wakati huo tayari timu hizo zimekwishafungana 2-2, mabao ya wenyeji, yakifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Afrika Kusini, Percy Tau dakika ya 17 na Roman Ferber dakika ya 71 na ya Genk yote yakifungwa na mshambuliaji Mbelgiji Zinho Gano dakika ya 47 na 75.
  Mbwana Samatta akisikitika baada ya kukosa penalti jana, KRC Genk ikitolewa Robo Fainali ya Kombe la Ligi Ubelgiji 

  Mshambuliaji Mghana, Joseph Paintsil (kushoto) akimfariji Mbwana Samatta baada ya kukosa penalti
  Na baadaya dakika ya 120, Samatta akaenda kukosa penalti ya pili kufuatia Gano kufunga ya kwanza na kiungo Mnorway Sander Berge akakosa ya nne, wakati penalti nyingine za Genk zilifungwa na kiungo Mspaniola Alejandro Pozuelo Melero na mshambuliaji Mghana, Joseph Paintsil.
  Penalti za Union Saint-Gilloise zilifungwa na Wafaransa Steven Pinto Borges, Faiz Selemani, Mbelgiji Kevin Kis na Tau huku beki Mbelgiji Pietro Perdichizzi pekee akikosa.   
  Samatta jana amecheza mechi ya tisa tu ya Kombe la Ubelgiji tangu asajiliwe KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na amefunga mabao mawili tu.
  Kwa ujumla, Samatta amekwishacheza mechi 135 katika mashindano yote Genk na amefunga mabao 53 – katika Europa League mechi 22 na kufunga mabao 14, wakati katika Ligi ya Ubelgiji amecheza mechi 104 na kufunga mabao 38. 
  Kikosi cha Union Saint-Gilles kilikuwa; Saussez, Perdichizzi, Hamzaoui/Selemani dk56, Pinto-Borges, Tabekou/Ferber dk67, Iriondo/Kis dk115, Morren/Moreno dk88, Niakate, Tau, Vega na Peyre.
  KRC Genk; Vukovic, Maehle, Aidoo, Lucumi/Dewaest dk91, Nastic, Berge, Seck/Samatta dk114, Piotrowski/Pozuelo dk46, Fiolic/Trossard dk59, Paintsil na Gano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AKOSA PENALTI GENK YATUPWA NJE KWA MATUTA KOMBE LA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top