• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 28, 2018

  TOFAUTI YA SIMBA SC NA WAPINZANI WAKE KUNDI D LIGI YA MABINGWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba ya Tanzania imepangwa Kundi D pamoja na JS Saoura ya Algeria, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Katika droo iliyopangwa usiku huu ukumbi wa Nile Ritz-Carlton mjini Cairo nchini Misri, Kundi A limezikutanisha timu za na Lobi Stars ya Nigeria, Wydad Casablanca ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
  Kundi B linaungwa na FC Platinums ya Zimbabwe, Horoya A.C ya Guinea, Esperance ya Tunisia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, wakati Kundi C limezikutanisha Ismailia FC ya Misri, CS Constantine ya Algeria, Club Africain ya Tunisia na TP Mazembe ya DRC.
  Mechi za hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa zitaanza Januari 11 mwakani na kufikia tamati Machi 17. Droo ya Robo Fainali itafanyika Machi 23, 2019.
  Simba SC wataanzia nyumbani Januari 11 dhidi ya J.S. Saoura kabla ya kusafiri kuwafuata AS Vita Januari 18 mjini Kinshasa na Al Ahly Februari 1 mjini Cairo kukamilisha mechi za mzunguko wa kwanza.
  Mzunguko wa pili itaanzia nyumbani Februari 12 dhidi yq Al Ahly mjini Dar es Salaam, kabla ya kusafiri kuwafuata J.S. Saoura nchini Algeria Machi 8 na kurejea nyumbani kumalizia na AS Vita Machi 15.
  Simba imefuzu tena kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 15, kufuatia mara ya mwisho kufika hatua hiyo mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Na msimu huu wamefuzu kwa kuitoa Nkana FC ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3, wakishinda 3-1 nyumbani baada ya kufungwa 2-1 ugenini.    
  Wakati mwaka 2003 ilifuzu ikiwa chini ya kocha Mkenya, James Aggrey Siang’a kipa wa zamani wa Harambee Stars, sasa marehemu, safari hii Simba SC imefuzu ikiwa chini ya kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems mwenye umri wa miaka 53, beki wa zamani wa Ubelgiji aliyechezea klabu za RCS Visé, Standard Liege, K.A.A. Gent, R.F.C. Seraing na ES Troyes AC.
  Na kabla ya Simba, Aussems amefundisha klabu za ES Troyes AC, SS Saint-Louisienne, Capricorne Saint-Pierre, Stade Beaucairois, Stade de Reims, KSA ya Cameroon, SCO Angers, Evian Thonon Gaillard F.C., Shenzhen Ruby, Chengdu Blades, AC Leopards ya Kongo na timu ya taifa ya Nepal.  
  Rekodi nzuri ya Simba SC Klabu Bingwa Afrika ni kufika Nusu Fainali mwaka 1974 ikiitoa Hearts Of Oak ya Ghana kabla ya kutolewa na Mehalla El Kubra ya Misri, lakini matokeo yake mazuri zaidi kwenye michuano ya Afrika ni kufika fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa na Stella Club Adjame, maarufu Stella Abidjan.
  Al Ahly ya Misri ni mabingwa mara nane wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika 

  AL AHLY
  Al Ahly Sporting Club, au National Sporting Club Kiingereza ni klabu yenye maskani yake katika mji wa Cairo, Misri. 
  Hii ni klabu bora ya Karne ya Afrika, iliyoanzishwa Aprili 24, mwaka 1907 na Umoja wa Wanafunzi mjini Cairo ikiwa na rekodi ya kutwaa mataji 40 ya Ligi Kuu ya Misri, vikombe 36 vya nchi hiyo, na mataji 10 ya Super Cup nchini humo yanayowafanya wawe klabu yenye mafanikio zaidi nchini humo. 
  Na kihistoria, Al Ahly yenye rekodi ya kutwaa mara nyingi taji la Ligi ya Mabingwa Afrika (mara nane), mataji sita ya Super Cup ya CAF, manne ya iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi Afrika, haijawahi kushuka daraja nchini humo
  Ahly pia ni washindi wa mataji ya Afro-Asian Club Championship, Arab Club Champions, Kombe la Washindi la Arab, na Arab Super Cup mara mbili ambayo pia ni rekodi na washindi wa Medali ya Shaba ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA mwaka 2006.
  Al Ahly ambao huvalia jezi za rangi nyekundu, bluu na nyeusi kwa sasa wapo chini ya kocha Martín Bernardo Lasarte Arrospide mwenye umri wa miaka 57, ambaye ni beki wa zamani wa Uruguay aliyewahi kuchezea klabu mbalimbali, ikiwemo Deportivo La Coruna ya Hispania kati ya 1989 na 1992.
  Amefundisha pia timu za Rampla Juniors, Rentistas, Bella Vista, Al Wasl, River Plate, Nacional, Millonarios, Danubio, Real Sociedad, Universidad Católica na Universidad Chile kabla ya Al Ahly.
  AS Vita ya Kinshasa ni washindi taji la Klabu Bingwa Afrika mwaka 1973

  AS VITA
  Association Sportive Vita Club, inayofahamika zaidi kama AS Vita Club, kifupi AS V. Club au tu Vita Club, hawa ni vigogo kabisa wa soka ya DRC wenye maskani yao katika Jiji la Kinshasa, klabu ambayo ilianzishwa na Honoré Essabe mwaka 1935 ikijulikana kwa jina la Renaissance.
  Mwaka 1939 ikabadilisha jina na kuwa Diables Rouges, kabla ya 1942 kubadilishwa tena na kuwa Victoria Club na hatimaye Vita Club mwaka 1971.
  Hao ni mabingwa wa Afrika mwaka 1973 na mabingwa mara 14 wa Ligi Kuu ya DRC, ijulikanayo kama Linafoot ambao kwa sasa wanaongoza Linafoot kwa pointi zao 56, wakifuatiwa na TP Mazembe yenye pointi 53 na DC Motema Pembe pointi 50 baada y azote kucheza mechi 22. 
  Timu hiyo ambayo huvalia jezi za rangi ya njano, kijani na nyeusi, kwa sasa ipo chini ya kocha Jean-Florent Ikwange Ibenge ambaye pia ni kocha Mkuu wa timu ya taifa ya DRC, akisaidiwa na kocha wa Yanga SC, Mwinyi Zahera.
  JS Saoura ni klabu mpya ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu

  JS SAOURA
  Jeunesse Sportive de la Saoura, au JS Saoura kwa urahisi, kifupi JSS ni klabu mpya ya mshambuliaji Mtanzania, Thomas Ulimwengu, yenye maskani yake katika mji wa Meridja jimbo la Bechar nchini Algeria, ambayo ilianzishwa mwaka 2008 tu na hutumia jezi za rangi ya kijani na njano kam Yanga ya hapa nyumbani.
  Wanatumia Uwanja wa Stade 20 Aout 1955, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 20,000 na kw asasa wanashika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Algeria, maarufu kama Ligue Professionnelle 1 ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 15, ikizidiwa pointi 10 na vinara, USM Alger.
  Mafanikio yao makubwa katika soka ya Algeria ni kuwa washindi wa pili wa Ligue Professionnelle 1 mara mbili katika misimu ya 2015–2016 na 2017–2018, ambayo iliwapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa.
  Inafundishwa na kocha mzalendo, Nabil Neghiz mwenye umri wa miaka 51, ambaye awali alifundisha timu za Mouloudia de Kaous, Entente de Collo, JS Djijel, MO Constantine, CRB Ain Fakroun, WA Tlemcen, Olympique de Médéa, Ohod na timu ya taifa ya Algeria kama kocha Msaidizi kati ya 2014 na 2017 na katikati mwaka 2016 alikuwa kocha Mkuu wa muda.
  Simba SC ilifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 na kutolewa na Mehalla El Kubra ya Misri

  TIMU GANI ZITAENDA ROBO FAINALI?
  Mechi za hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa zitaanza Januari 11 mwakani na kufikia tamati Machi 17 na timu mbili za juu katika kila kundi zitafuzu Robo Fainali ambayo itachezwa kwa mtindo wa mtoano. Droo ya Robo Fainali itafanyika Machi 23, mwakani 2019 ikifuatiwa na Nusu Fainali na baadaye Nusu Fainali.
  Ikumbukwe, kwa kufuzu tu hatua ya makundi kila timu itapata kitita cha dola za Kimarekani 190,000, zaidi ya Sh. Milioni 400 za Tanzania.
  Na kwa timu zitakazomaliza nafasi ya tatu zitapata dola 261,250, zaidi ya Sh. Milioni 600 wakati timu zitakazoingia Nusu Fainali kila moja itapata dola 427,500 zaidi ya Sh. Bilioni 1.
  Mshindi wa pili wa Ligi ya Mabingwa hupata dola 750,000, zaidi ya Sh. Bilioni 1. 5 na bingwa wa Afrika ataondoka kitita cha dola Milioni 1, zaidi ya Sh. Bilioni 3 za Tanzania.    
  Kutoka Kundi D, ni timu zipi zitakwenda Robo Fainali? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona kipute kitakapoanza. Kila la heri Simba SC. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TOFAUTI YA SIMBA SC NA WAPINZANI WAKE KUNDI D LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top