• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 28, 2018

  KAGERA YAICHAPA JKT, PRISONS YALAZIMISHWA SARE NA COASTAL SOKOINE

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  TIMU ya Kagera Sugar imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Omar Daga dakika ya 45 na kwa ushindi huo, Kagera Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Tanzania, Mecky Mexime inafikisha pointi 24 baada ya kucheza mechi 17 na kupanda hadi nafasi ya tano kutoka ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
  Mechi nyingine za leo, bao la dakika la dakika ya 90 la Hafidh Mussa liliinusuru Stand United kulala nyumbani mbele ya Alliance FC ya Mwanza iliyotangulia kwa bao la Dickson Ambundo dakika ya 24 na kupata sare ya 1-1 Uwanja wa Kambarage Shinyanga.
    
  Naye David Mwasa aliifungia Mbao FC dakika ya 90 ikinusurika kuchapwa na KMC iliyotangulia kwa bao la Emmanuel Mvuyekure dakika ya 45 na ushei nazo zikitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, wenyeji Tanzania Prisons wamelazimishwa sare ya 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi sita zaidi, Lipuli FC wakiikaribisha Ndanda FC Uwanja wa Samora mjini Iringa, African Lyon na Mwadui FC, Mtibwa Sugar FC na Azam FC Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mbeya City FC na Yanga SC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Ruvu Shooting FC na Biashara United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na Simba SC na Singida United FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGERA YAICHAPA JKT, PRISONS YALAZIMISHWA SARE NA COASTAL SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top