• HABARI MPYA

    Wednesday, December 19, 2018

    YANGA SC KUWAKOSA NYOTA WATANO WAKIWEMO FEISAL SALUM NA TSHISHIMBI MECHI NA AFRICAN LYON KESHO ARUSHA

    Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    VINARA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga SC kesho watawakosa nyota wake watano katika mchezo wa ugenini wa ligi hiyo dhidi ya wenyeji wahamiaji, African Lyon, zote za Dar es Salaam Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
    Mratibu wa Yanga SC, Hafidh Saleh ameiambia Bin Zubeiry amewataja wachezaji hao kuwa ni beki Andrew Vincent ‘Dante’, viungo Papy Kabamba Tshishimbi, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Raphael Daudi na Mrisho Khalfan Ngassa.
    Saleh amesema Dante na Daudi ni majeruhi, Tshishimbi amefiwa na baba mkwe wake hivyo amesafiri kwenda msibani, kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fei Toto anatumiki adhabu ya kadi tatu za njano na Ngassa atakuwa anamalizia adhabu yake ya kadi nyekundu.

    Papy Kabamba Tshishimbi amkwenda msibani DRC kufuatia msiba wa baba mkwe 

    Ikumbukwe Yanga pia itacheza mechi hiyo bila kocha wake Mkuu, Mwinyi Zahera ambaye amesafiri kwenda Ufaransa kwa mambo yake binafsi.
    Lakini beki mkongwe, Kelvin Yondan aliyekosekana kwenye mchezo uliopita Yanga SC ikishinda 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting kwa sababu ya adhabu ya kadi za njano anatarajiwa kurejea kesho.
    Wachezaji wapya, kipa Ibrahim Hamid na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ hawajasafiri na timu kwa sababu hawapo kwenye programu za mchezo huo,
    Yanga SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 44 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 40 baada ya wote kucheza mechi 16 na wanafuatiwa kwa mbali na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 27 za mechi 12.
    Simba SC leo wanateremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) katika mfululizo wa Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC KUWAKOSA NYOTA WATANO WAKIWEMO FEISAL SALUM NA TSHISHIMBI MECHI NA AFRICAN LYON KESHO ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top