• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 21, 2018

  ABDALLAH KHERI 'SEBO' KUWA NJE MIEZI TISA BAADA YA UPASUAJI AFRIKA KUSINI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Azam FC na timu ya taifa, Taifa Stars, Abdallah Kheri maarufu kama Sebo, atakuwa nje ya dimba kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia sasa baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti jijini Cape Town, Afrika Kusini.
  Kheri aliyerejea nchini usiku wa jana, mefanyiwa upasuaji huo baada ya kupata majeraha kwenye mchezo wa awali wa timu ya vijana ya Azam FC (Azam B), aliyokuwa akiichezea ili kujiweka fiti baada ya kutoka kuugua malaria, ambapo alidondokea mguu vibaya wakati alipokuwa akitoka juu kuokoa mpira.
  Daktari wa Azam FC, Dk. Mwanandi Mwankemwa, aliyeambatana naye nchini humo kushughulikia matatibabu yake, amesema kwamba beki huyo amekata mtulinga (ligament) wa kati na pembeni wa goti lake la mguu wa kulia na atarejea tena dimbani Agosti mwakani kwa ajili ya ushindani.


  Abdallah Kheri 'Sebo' (katikati) atakuwa nje kwamiezi tisa baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti nchini Afrika Kusini

  “Tarehe 14 (Desemba) alifanyiwa operesheni ya goti ambapo waliimarisha tena na kujenga upya mtulinga (ligament) wake wa kati na baadaye wakaunga ligaments zake za pembeni za goti lake la kulia na baada ya hapo ilibidi aonwe tena na daktari tarehe 18 ambapo alifunguliwa na kuangaliwa jeraha lake lipo vizuri na kuruhusiwa kurudi Tanzania,” alisema.
  Mwankemwa alizungumzia programu yake nzima ya matibabu kwa kipindi atakachokuwa yuko nje ya dimba, na kueleza kuwa beki huyo amevalishwa kifaa malumu kwenye goti lake (knee brace) kitakachotolewa baada ya wiki tatu kupita huku akipewa angalizo la kutokanyagia mguu wake kwa muda huo.
  “Wiki sita zitakazofuata atakifungua kile kifaa na kuanza kukanyagia mguu kidogo kidogo na baada ya wiki sita kupita ataanza kufanya mazoezi ya physio ya kuimarisha misuli ya paja ya mbele na ya nyuma na baada ya hapo akimaliza hizo wiki sita ataanza kufanya mazoezi ya baiskeli taratibu taratibu kwa muda wa miezi mitatu.
  “Baada ya hapo atakuwa na miezi mitatu mingine ya kukimbia na ‘jogging’, kwa hiyo Abdallah Kheri atarudi tena katika kucheza mpira baada ya miezi tisa kupita kwa hiyo inamaa Abdallah Kheri atarudi katika ushindani au kwenye mazoezi tena kama kawaida ya mpira mwezi wa nane mwakani (2019),” alimalizia programu hiyo.
  Baada ya ripoti hiyo inamaanisha kuwa mchezaji huyo bora wa Azam FC mwezi Septemba mwaka huu, anatarajia kuukosa msimu wote huu uliobakia na atareja msimu ujao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ABDALLAH KHERI 'SEBO' KUWA NJE MIEZI TISA BAADA YA UPASUAJI AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mwakasege Blog
  Scroll to Top