• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 26, 2018

  SIMBA SC YAPIGWA 3-2 NA MASHUJAA YA KIGOMA NA KUTOLEWA KOMBE LA TFF

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  VIGOGO, Simba SC wamerudia kutolewa mapema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kufungwa mabao 3-2 na Mashujaa FC ya Kigoma inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.    
  Msimu uliopita pia Simba SC walitolewa hatua kama hii ya 64 Bora na timu ya Daraja la Pili, Green Warriors ya Mwenge mjini Dar es Salaam, kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1, tena wakiwa mabingwa watetezi.
  Leo Simba SC waliuanza vizuri mchezo huo wakitangulia kwa bao la beki wake wa kati, Paul Bukaba Bundala aliyefunga dakika ya 18 akimalizia mpira uliopanguliwa na kipa Japhari Mtindi kufuatia shuti kali la kiungo Said Hamisi Ndemla.


  Lakini Mashujaa inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kama Green Warriors, wakasawazisha kupitia kwa Shaabani Hamisi dakika ya 47, aliyemtoka vizuri Bukaba kabla ya kumchambua kipa mkongwe Deo Munishi ‘Dida’.
  Jeremiah Josephat akaifungia Mashujaa FC bao la pili dakika ya 56 akimalizia kazi nzuri ya Mohammed Hajji aliyewatoka wachezaji wa Simba SC na kupenyeza pasi ya kiufundi kwa mbele.
  Bukaba akairudisha Simba SC mchezoni baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 78 akimalizia mpira uliogonga mwamba wa juu na kuanguka chini baada ya kupanguliwa na kipa Mtindi kufuatia shuti la mpira wa adhabu wa kiungo Mzambia Clatous Chama.
  Rajab Athuman akaimaliza Simba SC kwa kuifungia Mashujaa FC bao la tatu kwa shuti la umbali wa mita 21 dakika ya pili kati ya saba za nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo.
  Mechi nyingine ya ASFC leo, Mtibwa Sugar imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Kiluvya United Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, mabao ya Kelvin Sabato dakika za sita na 38 na Haruna Chanongo dakika ya 46.  
  Mbali na Mashujaa FC na Mtibwa Sugar timu nyingine zilizotinga hatua ya 32 Bora ni Yanga SC, Stand United, JKT Tanzania, Pamba SC, Biashara United, Mbeya City, Azam FC, Mbeya Kwanza, Kitayosce, Dodoma FC, Dar City, Lipuli FC, Singida United, Trans Camp, Pan African, Kagera Sugar, Friends Rangers, Rhino Rangers, Namungo FC, Reha FC, Majimaji FC, Boma FC, Cosmopolitan, Polisi Tanzania, KMC, La Familia, Coastal Union, Mighty Elephant na Alliance FC.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Zana Coulibaly, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Juuko Murshid, Muzamil Yassin/James Kotei, Shiza Kichuya, Said Ndemla, Adam Salamba, Abdul Suleiman/ Clatous Chama na Rashid Juma/Mohamed ‘Mo’ Ibrahim.
  Mashujaa FC; Japhari Mtindi, Shadrack Ntabindi, David David, Tryphone Guja, Enock Enock, Omary Mamba, Amani Amani, Masome Fares, Mohammed Hamisi, Shaaban Hamisi na Rajab Athumani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAPIGWA 3-2 NA MASHUJAA YA KIGOMA NA KUTOLEWA KOMBE LA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top