• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 19, 2018

  SIMBA SC KUMKOSA HASSAN DILUNGA MECHI NA KMC LEO TAIFA AMEFUNGIWA MICHEZO MITATU NA FAINI NUSU MILIONI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC itamkosa kiungo wake Hassan Dilunga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kufuatia kufungiwa mechi tatu.
  Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), maarufu kama Kamati ya Saa 72  imemfungia mechi tatu Dilunga pamoja na beki wa Lipuli FC ya Iringa, Ibrahim kwa kosa la kuchelewa kuondoka uwanjani baada ya kukamilika kwa dakika za kipindi cha kwanza.
  Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hizo Novemba 23, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam uliomalizika kwa sare ya 0-0 na wachezaji hao walitegeana kuondoka uwanjani baada ya kipindi cha kwanza.
  Hassan Dilunga hatakuwepo kwenye mechi na KMC leo jioni kufuatia kufungiwa mechi tatu 
        
  Sambamba na adhabu hiyo, wachezaji hao wawili kila mmoja ametakiwa kulipa faini ya Sh. 500,000 kabla ya kumaliza kifungo chao.
  Tayari Ibrahim Job, beki wa zamani wa Yanga SC alianza kutumikia adhabu yake kwenye mchezo uliopita wa timu yake wa ugenini dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Lipuli FC wakiibuka na ushindi wa 2-0.
  Simba SC yenye pointi 27 za mechi 12, inahitaji ushindi leo ili kuzifukuza timu zilizo juu yake katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, zinazoongozwa na Yanga SC wenye pointi 44 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 40 baada ya wote kucheza mechi 16.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUMKOSA HASSAN DILUNGA MECHI NA KMC LEO TAIFA AMEFUNGIWA MICHEZO MITATU NA FAINI NUSU MILIONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top