• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 19, 2018

  SIMBA WABUGIA KIPORO, WAITANDIKA KMC 2-1 NA KUWATIA ‘PRESHA’ YANGA KILELENI LIGI KUU

  Na Saada Salmin, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameonyesha bado wapo vizuri katika kulilinda taji lao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems, inafikisha pointi 30 katika mechi ya 13, sasa ikizidiwa pointi 14 na vinara, Yanga SC waliocheza mechi 16 wanaofuatiwa na Azam FC, zote za Dar es Salaam wenye pointi 40 za mechi 16 pia.   
  Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yakifungwa na mshambuliaji Adam Salamba na kiungo Said Hamisi Ndemla.

  Wachezaji wa Simba SC wakikimbia na Said Ndemla kushangilia baada ya kufunga bao la pili leo Uwanja wa Taifa

  Salamba alianza kuifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya 12 akimalizia pasi nzuri ya kiufundi ya kiungo mkongwe kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima kabla ya Ndemla kufumua shuti kutka nje ya boksi kufunga la pili dakika ya 14.
  KMC wakarudi nyuma baada ya bao hilo na kuanza kujilinda kuwazuia Simba SC kupata mabao zaidi jambo ambalo walifanikiwa kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza wakiwa wamefungwa mabao hayo hayo mawili. 
  Kipindi cha pili kocha Mrundi wa KMC, Etienne Ndayiragijje alianza na mabadiliko akiwapumzisha wote Abdul Hillary na Rehan Kibingu na kuwaingiza Reyman Mgungila na James Msuva.
  Mabadiliko hayo yaliizindua timu hiyo inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu ipande na kufanikiwa kupata bao moja, lililofungwa na Msuva, mdogo wa kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Msuva.
  James Msuva alifunga bao hilo akimalizia mpira uliotemwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’ kufuatia dhuti la Emmanuel Mvuyekure baada ya shambulizi lililoingizwa na Salum Chukwu.
  Pamoja na kufunga bao hilo, Msuva alimshughulisha zaidi kipa wa zamani wa Yanga na Azam FC, Dida kwa mashuti mawili ambao ‘yaliwarusha roho’ wapenzi wa Simba SC.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Zana Coulibaly, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Juuko Murshid, Muzamil Yassin, Said Ndemla, Haruna Niyonzima/James Kotei dk78, Adam Salamba/Meddie Kagere dk72, Rashid Juma/Clatous Chama dk60 na Shiza Kichuya.
  KMC; Jonathan Nahimana, Kelvin Kijiri, Salum Chukwu, Ally Ally, Yusuph Ndikumana, Ally Msengi, Abdul Hillary/Reyman Mgungila dk46, George Sangija/Sadallah Lipangile dk61, Elius Maguri, Emmanuel Mvuyekure na Rehan Kibingu/James Msuva dk46.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WABUGIA KIPORO, WAITANDIKA KMC 2-1 NA KUWATIA ‘PRESHA’ YANGA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top