• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 31, 2018

  YANGA SC YAAMUA KUWEKEZA NGUVU ZAIDI KWENYE LIGI KUU YA NA KOMBE LA TFF

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga SC ya Dar es Salaam imesema kwamba haitapeleka kikosi chake kamili kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, ili kuwapa mapumziko baadhi ya wachezaji wake.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema kwamba wanalazimika kuwapumzisha baadhi ya wachezaji kwa ajili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amesema kwamba, Yanga kama klabu inatakiwa kuweka malengo kwenye vitu vyenye manufaa kwake, kwani wakiamua kutaka mataji yote wanaweza kujikuta wanakosa yote.
  Kocha wa Yanga SC, Mwinyi Zahera (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo
    
  “Kufuatana na nguvu yetu tulionayo (wachezaji) inatubidi tuangalie wapi tutapata faida, tupo na Ligi Kuu, tupo na Azam Federation Cup, Mapinduzi Cup na Sport Pesa, inabidi sisi kama Yanga tuwe na malengo kwenye kitu chenye manufaa kwetu, tukiamua kuyataka makombe yote tunaweza kukosa yote, hivyo lazima baadhi ya wachezaji wapumzike kwa ajili ya Ligi na ASFC,” amesema Zahera ambaye pia ni kocha Msaidizi wa DRC.
  Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019 imepangwa kuanza kesho, Januari 1 hadi 13, mwakani ikifanyika katika miji ya Pemba na Unguja ikishirikisha timu tisa.
  Hizo ni KVZ, KMKM, Jamhuri, Chipukizi, Mlandege na Malindi kutoka Zanzibar na Azam, Simba na Yanga za Tanzania Bara.
  Kundi A linajumisha timu za Chipukizi, Mlandege, KMKM na Simba wakati Kundi B litakuwa na timu za KVZ, Malindi, Jamhuri, Azam na Yanga na kama ilivyo kawaida, mechi zote za mashindano hayo zitaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam kupitia chaneli zake mbalimbali.
  Bingwa wa Mapinduzi 2019 atajipatia kitita cha Sh. Milioni 15, ambazo ni ongezeko la Sh. Milioni 5 kutoka zawadi za mwaka huu, Mshindi wa pili atapata Sh. Milioni 10 badala ya Milioni 5 za msimu uliopita.
  Mechi zote za mashidano hayo msimu huu zitafanywa Uwanja wa Amaan uliopo Unguja hadi Nusu Fainali wakati mchezo wa Fainali utafanyika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba.
  Mechi za Amaan zitakuwa zinachezwa kuanzia Saa 10:15 jioni na Saa 2:15 usiku huku mechi ya fainali ikitarajiwa kuchezwa kuanzia Saa 9:30 Alasiri.
  Yanga itafungua dimba na KVZ Januari 3, kabla ya kumenyana na Azam FC Januari 5, Malindi Januari 7 mechi zote zikianza Saa 2: 15 usiku na kumalizia na Jamhuri Januari 9 kuanzia saa 10:15 jioni.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAAMUA KUWEKEZA NGUVU ZAIDI KWENYE LIGI KUU YA NA KOMBE LA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top