• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 29, 2018

  YANGA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA MBEYA CITY 2-1 SOKOINE

  Na Gwamaka Mwankota, MBEYA
  YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 2-1 Mbeya City katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Heritier Makambo kipindi cha kwanza, Yanga SC inafikisha pointi 50 baada ya kucheza mechi 18, ikishinda 16 na sare mbili.
  Sasa inawazidi kwa pointi 10, Azam FC wanaofuatia kwenye nafasi ya pili, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 30 za kuelekea mechi yao ya 14 ya msimu dhidi ya Singida United usiku huu, inafuatia katika nafasi ya tatu.  
  Makambo aliye katika msimu wake wa kwanza tu tangu asajiliwe Yanga SC, alifunga bao la kwanza dakika ya 16 kwa guu la kushoto akimalizia mpira adhabu uliopigwa na kiungo Ibrahim Ajibu.

  Bao hilo halikudumu sana, kwani Mbeya City walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wake hatari, Iddi ‘Nado’ Suleiman dakika ya 23 kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Kenny Kunambi.
  Lakini Makambo akavunja rekodi yake ya mabao katika mchezo mmoja, kwa mara ya kwanza akifunga mabao mawili siku moja baada ya kumalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kulia, Paulo Godfrey ‘Boxer’ kuipatia Yanga bao la pili dakika ya 41.
  Kipindi cha pili kiliuwa cha kosakosa kwa pande zote mbili, zaidi Yanga wakicheza kwa tahadhari ya kuulinda ushindi wao na Mbeya City wakipambana japo wapate sare.
  Lakini bahati ilikuwa ya Yanga kwa mara nyingine, wakifikisha mechi 18 za msimu huu wa Ligi Kuu bila kupoteza mechi na kupanua uongozi wao hadi pointi 10 dhidi ya Azam FC ambao leo wamepoteza mchezo wakichapwa 2-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.  
  Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Fikirini Barkari, Kenny Kunambi, Mpoki Mwakinyuke, Ibrahim Ndunguli, Erick Kyaruzi, Medson Mwakatundu, Iddi Suleiman ‘Nado’, Mohammed Samatta, Frank Ikobela, Mohammed Kapenta/Godfrey Milla dk85 na Eliud Ambokile/Peter Mapunda dk83.
  Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Ibrahim Ajibu/Pius Buswita dk85, Haruna Moshi, Heritier Makambo, Amissi Tambwe/Maka Edward dk72 na Mrisho Ngassa/Jaffar Mohammed dk75.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA MBEYA CITY 2-1 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top