• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 20, 2018

  SERENGETI BOYS YAPANGWA NA NIGERIA, ANGOLA NA UGANDA AFCON U17 DAR 2019

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WENYEJI, Tanzania wamepangwa na Nigeria, Angola na Uganda katika Kundi A Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) zitakazofanyika mjini Dar es Salaam kuanzia Aprili 14 hadi 28 mwakani.
  Katika droo iliyofanyika Mlimani City mjini Dar es Salaam leo, Kundi B linazikutanisha timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.
  Tanzania, Serengeti Boys itafungua dimba na bingwa mara mbili wa michuano hiyo, Nigeria Aprili 14 kabla ya kumenyana na Angola Aprili 17 na kukamilisha mechi za kundi lake kwa kumenyana na Uganda Aprili 20.
  Wazi Serengeti Boys wamepangwa kundi gumu na ili kwenda Nusu Fainali wajihakikishie kucheza Fainali za Kombe la Dunia nchini Peru kati ya Oktoba 5 na 27, mwakani wanahitaji kupambana kiume.
  Nigeria inapewa nafasi kubwa ya kuongoza Kundi na Tanzania itapigana na UIganda na Angola kuwania nafasi ya pili itakayowapa tiketi ya Peru mwakani.
  Katika Kundi B ni Cameroon, Morocco na Senegal zinapewa nafasi ya kugombea nafasi mbili za juu na Guinea wanachukuliwa kama wasindikizaji.
  Mapema mchana wa leo, wachezaji wa Serengeti Boys walikutana na Mlezi wa timu hiyo, mfanyabiashara Reginald Mengi na kula nao chakula cha mchana pamoja na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia katika hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.
  Na hiyo ni baada ya Serengeti Boys kutwaa ubingwa wa michuano ya U17 Kusini mwa Afrika baada ya ushindi wa penalti 6-5 dhidi ya Angola kufuatia sare ya bao 1-1, kwenye mchezo wa fainali mwishoni mwa wiki mjini Gaborone nchini Botswana.
  Na Serengeti Boys itashirki kwenye mashindano maalumu ya maandalizi ya Fainali za AFCON U17 mjini Antalya nchini Uturuki ambayo yameandaliwa na CAF kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) yataanza Februari 22 hadi Machi 2, mwakani na yakishirikisha jumla ya timu 12 kutoka Afrika na Ulaya.
  Mbali na Serengeti Boys nchi nyingine za Afrika zitakazoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Angola, Morocco, Cameroon, Uganda, Nigeria, Senegal na Guinea ambazo zitaungana na timu 4 kutoka Bara la Ulaya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAPANGWA NA NIGERIA, ANGOLA NA UGANDA AFCON U17 DAR 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top