• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 17, 2018

  ABDALLAH KHERI 'SEBO' KUREJEA DAR JUMATANO BAADA YA KUFANYIWA UPASUAJI WA KITAALAMU AFRIKA KUSINI MWISHONI MWA WIKI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Abdallah Kheri maarufu kama Sebo, mwishoni mwa wiki amefanyiwa upasuaji wa goti nchini Afrika Kusini.
  Kheri alifanyiwa upasuaji huo Ijumaa asubuhi baada ya kupata majeraha kwenye mchezo wa awali wa timu ya vijana ya Azam FC (Azam B), aliyokuwa akiichezea ili kujiweka fiti baada ya kutoka kuugua malaria, ambapo alidondokea mguu vibaya wakati alipokuwa akitoka juu kuokoa mpira.
  Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, aliyeambatana naye kwenye matibabu yake nchini humo, amesema kuwa upasuaji wa mchezaji huyo umemalizika salama katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town.
  “Upasuaji umeenda salama, tutakuja kumuona Dk. Nicholas Jumanne ijayo saa nne asubuhi, na siku hiyo tutaelekezwa programu ya matibabu yake (rehabilitation program) Inshallah Jumatano (19/12/2018) tutarejea nyumbani,” alisema.

  Abdallah Kheri 'Sebo' baada ya kufanyiwa upasuaji Ijumaa nchini Afrika Kusini

  Ripoti kamili ya atakuwa nje kwa muda gani pamoja na mambo mengine ya matibabu yake, yanatarajia kuwekwa wazi mara baada ya Mwankemwa kuonana na mtalaamu huyo.
  Daktari huyo wa muda mrefu wa tiba za wachezaji, alichukua fursa kutoa shukrani kwa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo kwa kufanikisha matibabu ya beki huyo, ambaye alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Azam FC mwezi Septemba msimu huu baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa.
  Wakati huo huo:Azam FC imemrejesha kiungo wake mkabaji Stephan Kingue, kwa mkataba wa mwaka mmoja na kufunga usajili wa dirisha dogo uliomalizika Jumamosi Saa 5:59 usiku.
  Kingue aliyekuwa amepumzishwa mara baada ya kupata majeraha kama ilivyokuwa kwa beki kisiki Daniel Amoah, ambaye naye amerejeshwa kwenye usajili wa dirisha dogo, anarejea akiwa fiti kabisa tayari kuendeleza mapambano.
  Aidha mbali na sababu za majeraha, wawili hao waliondolewa kwenye usajili wa dirisha kubwa Julai mwaka huu ikiwa ni kabla ya Azam FC kupata uhakika wa sheria ya kusajiliwa wachezaji 10 wa kigeni msimu huu, ambapo awali tulidhani ingeendelea ya ile ya wachezaji saba.
  Ujio wake ni sehemu ya kuimarisha eneo la kiungo cha ulinzi hasa baada ya Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, kuwa nje ya dimba kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti, hivyo kwa sasa atakuwa akisaidiana na viungo wa eneo hilo waliopo Mudathir Yahya na Salmin Hoza.    
  Usajili wa nyota huyo kutoka Cameroon unafikisha idadi ya wachezaji tisa wa kigeni waliokuwa kwenye kikosi cha Azam FC, kipa Razak Abalora (Ghana), mabeki Yakubu Mohammed, Daniel Amoah (Ghana), Bruce Kangwa (Zimbabwe), Nickolas Wadada (Uganda), winga Enock Atta (Ghana) na washambuliaji Obrey Chirwa (Zambia), Tafadzwa Kutinyu, Donald Ngoma (Zimbabwe).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ABDALLAH KHERI 'SEBO' KUREJEA DAR JUMATANO BAADA YA KUFANYIWA UPASUAJI WA KITAALAMU AFRIKA KUSINI MWISHONI MWA WIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top