• HABARI MPYA

    Sunday, August 12, 2018

    SIKU 365 ZA KARIA TFF NA TUHUMA ZA UNAZI WA SIMBA, KUONGOZWA NA MGOYI NA MENGINE MENGI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AGOSTI 12, mwaka jana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipata uongozi mpya, Wallace Karia akichaguliwa kuwa Rais kwa ushindi wa kishindo mjini Dodoma, akibeba kura 95 kati ya 128 zilizopigwa, huku aliyechukuliwa kama mpinzani wake wa karibu, Ally Mayay Tembele akiambulia kura tisa sawa na Shijja Richard.
    Wagombea wengine wa nafasi hiyo, Mwenyekiti wa zamani wa Yanga SC, Wakili Imani Madega alipata kura nane, Frederick Mwakalebela alipata kura tatu huku Emmanuel Kimbe akiambulia kura moja, wakati Michael Wambura alishinda nafasi ya Umakamu wa Rais.
    Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa Kanda 13 kwa mtiririko kuanzia Kanda Namba 1 ni; Saloum Chama, Vedastus Lufano, Mbasha Matutu, Sarah Chao, Issa Bukuku, Kenneth Pesambili, Elias Mwanjala, James Mhagama, Dunstan Mkundi, Mohamed Aden, Francis Ndulane, Khalid Abdallah na Lameck Nyambaya.
    Akitimiza mwaka mmoja madarakani leo, Bin Zubeiry Sports – Online ilikutana na Karia mjini Dar es Salaam kwa mahojiano juu ya safari yake ya siku 365 za awali katika awamu yake hii ya kwanza ya utawala wake. Endelea.

    Leo ni mwaka mmoja tangu Wallace Karia achaguliwe kuwa Rais wa TFF kwa ushindi wa kishindo, Agosti 12, mwaka jana mjini Dodoma

    Bin Zubeiry Sports – Online; Mheshimiwa Rais, unauzungumziaje mwaka wako wa kwanza wa kuwa kiongozi mkuu wa soka ya Tanzania?
    Wallace Karia; Ulikuwa mwaka mgumu, ingawa ninamshukuru Mungu nimeweza kutekeleza kwa kiasi nilichoweza yale niliyoahidi wakati ninaomba hii nafasi. Changamoto ni nyingi, kuna rasilimali fedha, watu kutokubali mabadiliko. Usimamizi wa fedha, vitu vyote vinakuwa na upinzani, lakini ninashukuru sehemu kubwa nimepata sapoti. Utaratibu wa fedha umeboreshwa, ulipaji wote sasa unafanyika kupitia benki na kwa uwazi na tunashughulikia masuala ya online banking. Utawala bora, ndani ya Sekretarieti kuna mabadiliko makubwa ya utendaji na yanaonekana. Kutatua matatizo haraka na kwa uwazi. Mawasiliano yamekuwa ya haraka na ya uwazi. Bado kuna changamoto za kufanyia kazi, kwa sababu asilimia kubwa ya watu ni wale wale niliowakuta.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kiufundi?
    Wallace Karia; Ufundi nako usimamzi wa mashindano umekuwa wa kuridhisha ligi zimechezwa kwa uadilifu, kwa sehemu kubwa waliokuwa wanastahili kushinda wameshinda, kuna changamoto mbalimbali tumezichkua na tunazifanyia kazi. Mafunzo ya utawala, ukocha na waamuzi yanafanyika vizuri tu. Kuna utaratibu wa mikutano ya kanda, tumefanya Magharibi, Kaskazini, Kati na wiki ijayo Kanda ya ziwa, baadaye Nyanda za Juu, Kusini na Mashariki. Kwa sababu kusubiri Mkutano Mkuu tuje tuwape taarifa, inaweza ikawa kuna vitu ambavyo tunahitaji mrejesho kutoka kwa wadau tukawa bado tunaendelea kuvikosea, kwa hivyo tumekuwa tunajadiliana nao, tunawaambia mwelekeo wetu, lakini pia tunapokea mrejesho na mawazo kutoka kwao. Hii inatufanya tukikutana katika Mkutano Mkuu inakuwa ni kwa ajili ya majumuisho tu.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kuna mpango mkakati labda?
    Wallace Karia; Ndiyo, Kiutaratibu taasisi haiwezi kuendelea bila kuwa na mpango mkakati, kwa hivyo ile ilani yangu ya kwenye uchaguzi, tumeibadilisha imekuwa kwenye mpango mkakati, ambao umegusa maeneo yote ambayo niliyazungumza, maeneo ya utawala, maeneo ya usimamizi wa fedha, usimamizi wa waamuzi, maeneo ya timu za taifa na maeneo ya Mawasiliano na Mahusiano. Kwa hivyo, vyote hivi tumevigusa kwenye mpango mkakati wetu ambao upo na tumesema kwamba tuutengeneze baada ya kuupitisha kwenye Kamati ya Utendaji ili tutoe nakala tuweze kuwapa wadau wetu wauone na ni mpango mkakati ambao tutakuwa tunaurekebisha kila muda kuendana na wakati na au kama kutakuwa kuna jambo linatokea katikati ambalo ni muhimu sana tuweze kurekebisha. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kuhusu timu za taifa?
    Wallace Karia; Kwenye mpango mkakati tumetaja usimamizi mkubwa wa timu za taifa, nadhani ni mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 12 sasa timu zote za taifa zimeshiriki katika mashindano yote ambayo tulistahili kushiriki. Lakini wenyewe mmeona, katika mashindano hayo ingawa tumeshiriki yote, tumefanikiwa kupata vikombe viwili (CECAFA Challenge U17 na wanawake). Lakini bado tuna mashindano ambayo yanaendelea ya timu yetu ya taifa ya wakubwa (Kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika), tumejipanga kwamba ni lazima nayo tufaye vizuri. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ndani ya mwaka mmoja mmefanya mambo mengi sana
    Wallace Karia; Kweli, hayo yote tumeyafanya katika kipindi hiki cha mwaka mmoja kwa hali ngumu sana. Ukosefu wa fedha, unajua kabisa shirikisho letu limezuiwa na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kupata ruzuku ya maendeleo, lakini pia na wadhamini tuliokuwa nao kutotosheleza hali halisi ambayo ipo. Kwa hivyo, hilo ni changamoto ambayo tumekutana nayo na tunajitahidi kwamba ikiwezekana tuondokane nalo, kwa hivyo tuna mipango mingi.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Vipi kuhusu Idara ya Masoko? 
    Wallace Karia; Tumeimarisha kitengo chetu cha Masoko, lakini pia tumekuwa na mawasiliano mbalimbali na wadau kuhakikisha kwamba angalau tunapata uwezo wa kugharamia mahitaji yetu ambayo yametusimamia.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kuhusu Utawala Bora?
    Wallace Karia; Mwaka huu mmoja pia ni mwaka ambao tumesimamia utawala bora kwa kiwango ambacho tumeona kinaridhisha. Katika kipindi hiki tumechukua hatua mbalimbali za kiutawala bora katika maeneo ambayo tuliona kwamba yanahitaji kuchukua hatua hizo ili tusije tukarudi tena kule kule ambako kulikuwa na usimamizi mbaya wa masuala ya fedha, ingawa imetuletea changamoto nyingi sana, kwa sababu mnapofanya hivyo, kuna ambao hawakubaliani na ambayo yanatokea, lakini tumeyafanya kwa nia njema kabisa na hatukuweza kuonea mtu yeyote, lakini tu bado tunazungumza kwamba, sisi tunasimamia katika utaratibu na tutaendelea kusimamia katika utaratibu huo ili kuhakikisha angalau imani inarudi kwenye taasisi yetu na kuweza kuwavutia wadau na wawekezaji mbalimbali kwenye taasisi yetu.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ulitoa ahadi ya kugawa fedha mikoani kwa ajili ya miradi ya maendeleo, umetekeleza?
    Wallace Karia; Hatujaweza kutekeleza ahadi ya kupeleka fedha kwenda chini, kwenda mikoani kuimarisha ofisi zao na kusimamia ofisi zao na kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo, tumelifanya kwa kiasi kidogo sana, kwa sababu bado hizo fedha hatujazipata.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Miundombonu?
    Wallace Karia; Miundombinu tumejitahidi, tumekwishatengeneza michoro, tumeigharamia ya kituo chetu cha Ufundi cha Karume na kituo chetu cha Ufundi cha Tanga, lakini tuna jitihada mbalimbali tunazifanya za kuweza kusaidiana na wadau wetu kuboresha miundombinu haswa ya viwanja vya kuchezea mpira, ili viweze kuwa katika hali nzuri ya kuchezea mpira. Mfano tumeshirikiana na wenzetu wa CCM (Chama cha Mapinduzi) na tunaendelea kushirikiana kuboresha Uwanja wa Jamhuri, kuboresha Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, lakini pia tumeshirikiana na Serikali ya wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi, kuweza kuunga mkono juhudi za Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) za kutengeneza Uwanja katika mkoa wa Lindi katika eneo la Ruangwa. Lakini pia tumekuwa na mazungumzo mbalimbali na baadhi ya wakuu wa mikoa kuangalia ni jinsi gani ya kuweza kuboresha miundombinu ya viwanja ili kuweza kupata sehemu za vijana wadogo kuweza kufanya mazoezi. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Mikoa ipi kwa mfano?
    Wallace Karia; Kwa mfano mkoa wa Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, tumeshirikiana nao kwa karibu sana. Lakini pia tunaendelea na juhudi za kutaka kushirikiana na taasisi za Serikali kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambacho kina miundombinu mingi kuingia nao katika makubaliano ya kuturuhusu kutumia miundombinu yao ya viwanja, ili kuweza kuweka programu zetu za vijana. Tumeshirikiana bado na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye michezo yake ya UMITASHUMTA na UMISETA kuhakikisha kwamba tunapata vipaji vile na kuviendeleza, ili kuwe na mlolongo wa kupata vijana kila hatua, wanaotoka U20 wanaenda U23, wanaenda timu ya wakubwa, tunapata wengine wale waliokuwa U17 wanaenda U20, waliokuwa kwenye U13 wanaenda U15.   
    Bin Zubeiry Sports – Online; Vipi kwa klabu za Ligi Kuu na madaraja mengine, programu ya vijana imetekelezwa?
    Wallace Karia; Tumetoa maelekezo kwa klabu za Ligi Kuu msistizo wa mashindano ya vijana, ni sheria kila timu ya Ligi Kuu lazima iwe na timu ya kuanzia U14 lakini katika mashindano kutakuwa na ligi za U17 na U20, kwa hivyo timu za Ligi Kuu lazima ziwe na timu za U17 na U20 ambazo tutazisajili na za Daraja la Kwanza lazima ziwe na U17 ambayo pia tutaisajili ili iweze kushiriki ligi. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Itaendelea kuwa Ligi ya wiki mbili mbili vituoni?
    Wallace Karia; Hapana, kuanzia sasa hivi tutakuwa na Ligi kamili ya nyumbani na ugenini kwa timu za U20 za Ligi Kuu peke yake, na tutakuwa na Ligi ya pamoja ya U17 ya timu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na la Pili.  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ni kweli kuna mpango wa kufufua Kombe la Taifa? 
    Wallace Karia; Ndiyo, tunataka turudishe mashindano ya Taifa Cup, sambamba na mfumo wa U15 ambao tutakuwa tunaucheza kama ulivyokuwa mfumo wa Copa Coca Cola, kwa hivyo katika yote hayo ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na utaratibu mzuri wa kuweza kupata vijana, muongozo kuhusu Taifa Cup tutautolea maelezo baadaye.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kuhusu mashindano mengine, ikiwemo Kombe la TFF?
    Wallace Karia; Tutaboresha mashindano yetu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), yataongeza timu zaidi ili yaweze kuwa na msisimko na ushindani zaidi 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kumekuwa na migogoro ya ndani ya shirikisho ndani ya muda huu mfupi, kiasi cha Makamu wako (Wambura) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (Clement Sanga) kuondolewa madarakani huku wakilalamika kufanyiwa fitina. 
    Wallace Karia; Mimi nimesema huwa tunasimamia utawala bora, binadamu yeyote haachi kulalamika, lakini ni vizuri tu nisilizungumzie sana hili kwa sababu mengine bado yapo kwenye michakati ya kukata rufaa, lakini hatujaonea mtu. Tumekwenda katika utaraibu tu mzuri na nyinyi waandishi nyie ndio mtusaidie nyie ndio muwaulize.  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Suala la Sanga limekaa vipi, labda la Wambura lipo kwenye vyombo vya Sheria
    Wallace Karia; Suala la Sanga, mimi haya mambo sipendi kuyaongelea sana, lakini hili suala liko wazi sana, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi anatakiwa awe Mwenyekiti wa klabu, Yanga wametuletea barua kwamba Sanga si Mwenyekiti wao, na hicho kikao ambacho kimesema Sanga si Mwenyekiti wa Yanga, Sanga mwenyewe alikuwa anakisimamia.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Umeingia madarakani baada ya viongozi waliokuwepo kuwekwa rumande kwa tuhuma na ubadhirifu – pamoja na haya yanayoendelea, unadhani picha ya shirikisho ikoje machoni mwa wadau?
    Wallace Karia; Ni picha nzuri kwa sababu wanajua tupo makini na usimamizi wa rasilimali fedha, lakini pia katika kipindi changu hakujatokea ubadhirifu, sisi kama taasisi tumepokea taarifa za ukaguzi za miaka ya nyuma, ambazo zilitakiwa zijadiliwe katika kipindi hiki na ndiyo tumeona hayo mapungufu ambayo yametokea ya kifedha, kwa hivyo tumechukua hatua, hatukufunika na tulikuwa wazi, na wenyewe walipewa tuhuma hizo. Na niseme tu, kwa yeyote atakayefanya mchezo na rasilimali fedha tutamuondoa kwenye familia ya mpira, kwa sababu tunataka watu wajenge imani na sisi na wajue kwamba kama wakileta rasilimali fedha zao zinatumika kwa njia ambayo inastahili.    
    Bin Zubeiry Sports – Online; Desemba mwaka jana mliingia mkataba wa udhamini wa jezi za timu za taifa na kampuni ya Macron, lakini hadi sasa hatujaona dalili za mkataba huo kufanya kazi. Vipi?
    Wallace Karia; Suala la Macron nalo lipo kwenye masuala ya kisheria na mkataba huo hatukusaini sisi tu, kuna baadhi ya klabu nazo zilisaini. Na kama unavyojua sisi tunahitaji wadau mbalimbali wa kuweza kufanya nao kazi, sasa kumetokea kidogo sintofahamu ya kisheria ambayo siwezi kuiongelea kwa sababu hilo suala lipo katika masuala ya kisheria
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kwenye mikono ya sheria, nyinyi ndiyo walalamikaji, au walalamikiwa?
    Wallace Karia; Kwenye mkataba kulikuwa kuna vipengele vinavyoelekeza kama ikitokea mmoja hakutekeleza masharti ya mkataba kuna hatua za kufuata, kwa hivyo ndivyo tunazifuata hizo hatua.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kukwama kwa dili la Macron kumepunguza nini katika hazina ya timu za taifa?
    Wallace Karia; Kama nilivyozungumza tuna tatizo la rasilimali fedha, lakini miaka ya nyuma tulikuwa tunaambiwa baadhi ya timu tu ndiyo zishiriki ili ziweze kufanya vizuri, lakini mbali ya kwanza tuna changamoto hizo mwaka huu timu zote tumeziingiza kwenye mashindano na zimecheza vizuri kwa baadhi ya timu na hata nyingine ambazo zimetoka ni kimchezo tu, kwa hiyo hili halijatuathiri kwa sababu tumejipanga.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Tukibaki kwenye suala la Taifa Stars, kipi kimewashawishi kumchukua kocha Emmanuel Amunike?
    Wallace Karia; Sisi tunatafuta mtu ambaye tunahisi kwamba atatufikisha kule ambako tunastahili na ndiyo tumeona kwamba yeye ndiye anatufaa, inawezekana wakawa wapo wengi, lakini kwa jicho letu sisi na mazungumzo, ndiyo ambaye ameelekea na tumekubaliana naye na ni jambo ambalo halina mjadala kwa Emmanuel Amunike na malengo yetu ambayo tunataka ni kuwa na sisi hapa 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Agosti 22, ikitanguliwa na mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 18, lakini hadi sasa kuna sintofahamu ya mdhamini mkuu. Hili unalizungumziaje?
    Wallace Karia; Mimi nadhani kwa sababu tu miaka ya karibuni hali ya mawasiliano imekuwa kubwa zaidi na kila mtu anajua kitu gani kinafanyika kwa uwazi na uwazi tuliokuwa nao, ndiyo maana inazungumzwa hivyo, lakini miaka mingi mkataba wa Vodacom unapofikia mwisho, unakuta dakika za mwsho ndiyo tunaingia kusaini nao mkataba. Kwa hiyo niseme bado tupo kwenye mazungumzo nao, kuna vitu bado hatujakubaliana ndiyo maana tumechelewa kutangaza mkataba mpya.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Lakini siku zimebaki chache mno kiasi cha kuanza kutia wasiwasi, nini kinawachelewesha? 
    Wallace Karia; Tumesema kabisa kwamba wakati tunaingia madarakani tutahakikisha kwamba mikataba iwe katika utaratibu ambao angalau utakuwa na tija kwetu sisi pamoja na wadau wetu ambao ndiyo tunaingia nao mkataba, kwa hiyo ndiyo hayo ambayo tunayazungumzia, lakini mimi nina imani kubwa kabisa kwamba Ligi bado itapata mdhamini, na kuna uwezekano mkubwa tukaendelea na Vodacom. Lakini anaweza akawa na wenzake wengi, ambao watasaidiana naye, ni utaratibu wetu pia tumeona kwamba ikiwezekana tusiwe na mdhamini mmoja ambaye tunampa udhamini mkuu wakati bado hatupati kile ambacho tunakiona kwa thamani hiyo ya udhamini mkuu. Tutaangalia si ajabu tukawa na wadhamini wengi tu, mmojawapo akawa Vodacom.   
    Bin Zubeiry Sports – Online; Klabu zetu kukamilisha taratibu za msingi (Club Licensing) zinazotakiwa na CAF na FIFA, kama kuwa na Uwanja wake maalum wa mazoezi na mechi, timu rasmi za vijana inaonekana bado tuna safari ndefu sana
    Wallace Karia; Inaonekana kuna safari ndefu kwa sababu tunaleana, lakini kusema ukweli sisi tutalisimamia kwa karibu sana na sehemu kubwa ya Club Licensing mwaka huu itatekelezwa na Kamati (ya kushughulikia Club Licensing) inafanya kazi zake, kuna changamoto nyingi, lakini hili litafikia mwisho. Lakini kwenye Club Licensing kuna vitu vya kufanyika wakati huo huo, na kuna vingine vina muda mtu anapewa avifanye, kwa hiyo. Vile vingi vya kufanyika muda huo huo, tayari vingi tumekwishavifuatilia na vile vingine sasa ambavyo vinapewa muda, tutautoa muda na huo muda utakapotolewa hautakuwa na hiari yoyote, lazima utekelezwe.     
    Bin Zubeiry Sports – Online; Tutakuwa wenyeji wa AFCON U17 mwakani matayarisho yamefikia wapi? 
    Wallace Karia; Matayarisho yanaenda vizuri, wakaguzi walikwishakuja, wameangalia miundombinu, wameridhishwa na miundombinu, na sehemu kubwa ya matayarisho ni mashindano haya ambayo tunayaanza Agosti 11 (jana), tupo katika kujipima na ndiyo maana tumeyaleta, katika zile changamoto tutakazoziona ndiyo tutazirekebisha kwa ajili ya mashindano yajayo.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Vipi kuhusu maandalizi ya timu
    Wallace Karia; Maandalizi yako vizuri sana. Kulikuwa pia kuna mashindano ya Algeria. Hatukwenda kwa sababu Olimpiki Afrika na CAF walishindwa kuafikiana, kwa hiyo sisi ambao tulipitia CAF imebidi tusishiriki yale mashindano.  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kulikuwa kuna habari za kwenda kuweka kambi Sweden
    Wallace Karia; Safari ya Sweden nayo ilikuwa ina changamoto zake za kiufundi, tumeona kwamba angalau tukaangalia wakati mwingine kwa hawa vijana ambao tulikuwa nao ilionekana kwamba hawawezi kwenda Sweden katika kipindi hiki, labda baada ya mashindano haya yanayofanyika, kwa hiyo tutaangalia sehemu nyingine baada ya mashindano haya. Lakini matayarisho yako vizuri kabisa na tumempata mkuu, ambaye atashughulika na timu zote. Amunike, mbali na kuwa kocha wa timu ya wakubwa, atakuwa kocha wa timu zote.  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kim Poulsen hayupo tena, Oscar Milambo ni Mkurugenzi wa Ufundi, nani sasa ni kiongozi wa benchi la Ufundi la Serengeti Boys?
    Wallace Karia; Kwa kipindi hiki ambacho Kim Poulsen hayupo, bado Oscar ndiye alikuwa anasimamia timu na ataenda nayo kwenye mashindano haya akishirikiana na Amunike, baada ya mashindano haya, mwalimu (Amunike) ataangalia utaratibu gani mpya
    Bin Zubeiry Sports – Online; Walimu gani wapo na timu kambini Azam Complex, (Chamazi, Dar es Salaam)
    Wallace Karia; Yupo Oscar Milambo, Peter Manyika (kocha wa makipa) na Meneja Kenneth Mkapa.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Hamuoni umefika wakati wa kuacha kutumia makocha wa klabu na muwe na makocha wenu wenyewe, mfano Bakari Shime ni kocha wa JKT Tanzania, nanyi mnamtumia katika timu ya wanawake. 
    Wallace Karia; Timu za taifa siyo za kudumu, hazifanyi mazoezi wakati wote wa msimu, wanapokuwepo inawasaidia wao kupata uzoefu zaidi na utaalamu 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ongezeko la idadi ya wachezaji wa kigeni Ligi Kuu kutoka saba hadi 10, wengi hawajaafiki akiwemo Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga 
    Wallace Karia; Mimi ndiye naongoza TFF, hata kama kesho nitaondoka mimi siyo kamusi ya mpira, kila mmoja ana mtazamo wake na mwelekeo wake. Mimi nadhani hakuilalamikia, amesema litazamwe na tumekwishasema kwamba tutalitazama, lakini kanuni tumekwishapitisha, siyo Rais Tenga tu aliyezungumza, hata Mheshimiwa (Dk. Harrison) Mwakyembe (Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo) alizungumza na tunawaheshimu sana. Lakini pia wao wenyewe wanajua kuna masuala ya utawala bora na hili suala limetokea wapi na michakato ipi, viongozi wetu, wazee wetu wametuambia tumeyachukua, tutalifanyia kazi, lakini na wao pia waliangalie katika jicho lingine, kwa sababu mimi ninadhani uoga ni kwamba labda tungekuwa na wachezaji 200 (wa kigeni), 10 mara 20, hapana, maombi hayajazidi hata asilimia 10. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Wasiwasi ni kwamba katika timu kubwa watasheheni wachezaji wa kigeni, maana yake timu ya taifa itaundwa na wachezaji wengi wa timu zinazopigania kuepuka kushuka daraja
    Wallace Karia; Kwanza, mtazamo wa kidunia lazima tuufuate, sisi siyo kisiwa. Sisi mtazamo wetu ni kuhakikisha wachezaji wetu wa Tanzania wanakwenda kucheza Ligi za nje na wengi wao watakaokuwa wanacheza ligi za nje ndiyo watakaokuwa wanachezea timu ya taifa kwa kushirikiana na wale ambao wapo vizuri ambao wanacheza ligi ya ndani. Tumekwishakaa hivyo miaka mingi tangu tumepata Uhuru tunategemea wachezaji wanaocheza ligi ya ndani, hatukuweza kufanikiwa, kwa hiyo tunaomba wao watupe muda, kwa sababu sisi ni viongozi na tuna mtazamo wetu. Watuache na mtuache tupange kazi zetu mje mtuadhibu au mtupime kwa mafanikio ambayo tutayapata au katika makosa ambayo tutakuwa tumeyafanya.   
    Bin Zubeiry Sports – Online; Maoni ya wengi ni kuwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa kigeni mwenye elimu na uzoefu mkubwa ambaye atakuja kututengenezea programu nzuri zaidi ya hizi tulizonazo 
    Wallace Karia; Ni maoni yao, lakini na sisi kama taasisi tuna mtazamo wetu. Na suala hilo tunalifanyia kazi, sasa hivi Oscar Milambo anakaimu. Si ajabu tukasema Oscar ambaye ni kijana ana elimu nzuri na amekwishakwenda kushiriki kozi mbalimbali nje na ni Mtanzania ambaye tunataka tumuwezeshe ili aweze kufanya na ndiyo maana tumempa nafasi hiyo kwa sababu bado ni kijana mdogo na tuna uwezo wa kuendelea kumuwezesha aweze kupata mawazo mapya. Tutakapoona kuna haja kweli ya kuleta mgeni, sawa.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Katika mwaka wako wa kwanza, umezungumzia changamoto ya rasilimali fedha na sababu kubwa ni FIFA kusitisha kuleta fedha za ruzuku kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Je, hilo limefikia wapi kwa sasa?
    Wallace Karia; Sasa hivi tupo katika hatua za mwisho mwisho, na labda nikuambie mojawapo ya masharti ni kuhakikisha kwamba tunachukua hatua kwa wale wote ambao walikuwa wana ukosefu kwenye fedha na masuala mengine mengi tu ambayo sasa hivi tupo katika hatua za mwisho katika kukamilisha  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Matarajio ni kuanzia lini mtaanza tena kupata fedha za FIFA
    Wallace Karia; Sisi tuna uhakika kwamba haitafika Desemba mwaka huu hatujaanza kupata tena fedha hizo, na kwa hali ambayo tumeonyesha tutapata na zile ambazo pia hatukuzipata miaka iliyopita 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kiasi gani cha fedha ambacho hadi sasa mnastahili kupewa FIFA pamoja na malimbikizo?
    Wallace Karia; Kiasi ambacho hakikuja ni dola Milioni 3 (za Kimarekani) ambazo ni za maendeleo, hizi nyingine wanatuletea kutokana na utaratibu ambao wametuwekea wao
    Bin Zubeiry Sports – Online; Umesikia maneno kwamba TFF hii ni ya Kisimba, Simba, Rais Simba, Katibu Simba na Wajumbe wengi kadhalika?
    Wallace Karia; Kwa nini hawajasema Coastal (Union). Kwa sababu kiongozi mkuu wa TFF wa sasa ni Coastal, kwa hiyo TFF basi ni Coastal. Lakini haijalishi kwamba pale yuko nani na ana asili gani, kinachojalisha ni utekelezaji. Nikuulize wewe swali, je katika kipindi chetu ulichoona, kuna mtu ambaye amenyimwa haki yake?
    Bin Zubeiry Sports – Online; Na hili la kwamba wewe unaongozwa kwa rimoti (remote control) na mmoja wa Wajumbe wako, Ahmed Iddi, maarufu Msafiri Mgoyi? 
    Wallace Karia; Kwanza niwaambie kwamba, hayo mazungumzo hayajaanza leo, yameanza tangu wakati wa Tenga, yamekuwepo tangu wakati wa Malinzi (Jamal, Rais aliyemfuatia Tenga TFF na ambaye amemuachia kiti Karia). Sasa kwa nini wenyewe msijiulize, kwa nini Mgoyi, wako Wajumbe wengi, na kuna watu walikuwepo tangu Serikali ya Nyerere (Mwalimu Julius Kambarage, rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania), Serikali ya Mwinyi (Ali Hassan, Rais wa pili), Serikali ya Mkapa (Benjamin William, Rais wa tatu), Serikali ya Kikwete (Jakaya Mrisho, Rais wa Nne) na bado wengine wapo hadi leo katika Serikali ya Magufuli. Kwa hiyo kila kiongozi anataka afanye jema na ashirikiane na mtu ambaye ni mwema na mtu ambaye anamsaidia. Mimi Mgoyi ananisaidia sana na ni mwepesi kuliko Wajumbe wangu wengi wa Kamati ya Utendaji. Lakini yupo karibu na mimi, yupo Dar es Salaam, lakini pia ninamuamini.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Inasemwa semwa, Karia ameletwa na Serikali kuongoza mpira wa Tanzania, na wewe ni mtumishi wa Serikali (TAMISEMI)
    Wallace Karia; Hapana, mimi nimeajiriwa kazi mwaka 1990. Na mwaka huo huo 1990 nilikuwa kiongozi Coastal Union, sikutumwa, ni utashi wangu ambao umenituma kwa mapenzi yangu ya mpira, lakini pia kwa kuona kwamba naweza. Na nilianza ngazi za chini za uongozi hadi kufika juu. Na ndoto zangu ni kuwa kiongozi wa bodi nyingine kubwa za soka CECAFA, CAF hadi FIFA. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Mheshimiwa Rais, kwa mwaka wa kwanza, niseme inatosha nikuachie nafasi uingie katika mwaka wa pili wa uongozi wa TFF.
    Wallace Karia; Asante. Nikutakie kazi njema na wewe katika majukumu yako ya kila siku. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIKU 365 ZA KARIA TFF NA TUHUMA ZA UNAZI WA SIMBA, KUONGOZWA NA MGOYI NA MENGINE MENGI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top