• HABARI MPYA

    Monday, October 17, 2016

    AZAM NA MTIBWA KUPIGWA USIKU JUMATANO CHAMAZI

    Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar ya Morogoro utafanyika usiku wa Jumatano Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 
    Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kwamba wameomba mchezo huo ufanyike usiku na wanashukuru ombi lao limekubaliwa na Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    “Wenzetu wa Azam TV kwa sababu za kuweza kuonyesha moja kwa moja mechi nyingi za Jumatano, wakaomba mchezo wetu tuusogeze Saa 1:00 usiku, nasi tumekubali,” amesema Maganga.
    Azam iliyo chini ya benchi la Ufundi la wataalamu kutoka Hispania linaloongozwa na Zeben Hernandez Rodriguez, itaingia katika mchezo wa keshokutwa ikitoka kutoa sare ya 0-0 na Yanga jana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Azam FC inafikisha pointi 12 baada ya kucheza mechi tisa, ikitoa sare ya tatu baada ya kufungwa mechi tatu na kushinda tatu – wakati Simba SC yenye pointi 23 za mechi tisa kutokana na kushinda mara saba na sare mbili, inaongoza Ligi Kuu.
    Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Jumatano na mbali na Azam na Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Ndanda FC wataikaribisha Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Prisons watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
    Mechi nyingine za Jumatano, Toto Africans watawakaribisha baba zao, Yanga SC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, African Lyon wataikaribisha Maji Maji Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Alhamisi Simba SC watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Uhuru na JKT Ruvu wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mabatini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM NA MTIBWA KUPIGWA USIKU JUMATANO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top