• HABARI MPYA

  Friday, October 28, 2016

  MWIGULU AMRUDISHA KAZINI PLUIJM YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imemuandikia barua ya kumjibu kocha wake, Mholanzi Franciscus Johannes ‘Hans’ van der Pluijm juu ya ombi la kujiuzulu ikitaa ombi hilo.
  Katika barua iliyosainiwa na Katibu, Baraka Deusdedit, Yanga imesema haioni sababu ya kuachana na Mholanzi huyo baada ya mafanikio aliyoipa klabu.  
  Mholanzi huyo alijiuzulu mapema wiki hii baada ya kukerwa na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima.
  Kocha huyo akakataa hadi nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi amabyo inasemekana Yanga ilitaka kumpa baada ya kumleta Lwandamina kuwa kocha Mkuu.
  Waziri Nchemba (kulia) akizungumza na kocha Pluijm kumshawishi arudi kazini
  Waziri Nchemba (katikati) akizungumza na kocha Pluijm (kulia) na Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit 
  Lakini baada ya kuwaaga wachezaji siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu timu ikishinda 4-0, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliingilia kati suala hilo.
  Waziri Mwigulu ambaye ni mpenzi na mwanachama wa Yanga, kwanza aliushauri uongozi kumrudisha Pluijm na baadaye akaenda kuzungumza na kocha huyo pia kumshauri akubali kurejea.
  Baadaye akazikutanisha pande zote mbili, Pluijm na uongozi wa Yanga katika kikao ambacho inaelezwa makubaliano yalifikiwa.
  Leo uongozi wa Yanga umemuandikia barua Pluijm kumuomba rudi kazini na inasemekana Mholanzi huyo anaweza kushiriki mazoezi ya jioni Uwanja wa Uhuru leo timu ikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao Jumapili.
  Uongozi wa Yanga ulitaka kumuondoa Pluijm na Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo na kuwaleta Mzambia Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  
  Pluijm, aliyezaliwa Januari 3 mwaka 1949, alikuwa anafundisha Yanga katika awamu ya pili baada ya awali kufundisha kwa nusu msimu mwaka 2014, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts.
  Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana. 
  Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.
  Pluijm alitaka kuondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 124, akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22.
  Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 106 za tangu mwaka jana, alisema 66, sare 19 na kufungwa 20.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWIGULU AMRUDISHA KAZINI PLUIJM YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top