• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 22, 2016

  YANGA WAANZA LIGI, WAIPIGA KAGERA 6-2…CHIRWA 2, NGOMA 2, MSUVA MOTO CHINI

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  YANGA wameanza rasmi mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara – baada ya leo kuwatandika wenyeji Kagera Sugar mabao 6-2 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Ushindi huo wa kwanza mkubwa zaidi msimu huu, unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 21 baada ya kucheza mechi 10 na kupanda hadi nafasi ya pii, nyuma ya Simba SC yenye pointi 26. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Suleiman Kinugani aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha na Nicholas Makalanga, hadi mapumziko Yanga walikuwa wanaongoza 3-1.
  Wafungaji wa mabao ya Yanga kutoka kulia Obrey Chirwa, Donald Ngoma na Deus Kaseke wakipongezana

  Na mabingwa hao watetezi, walilazimika kutoka nyuma baada ya Mbaraka Yussuf kutangulia kuifungia Kagera Sugar dakika ya tatu.
  Mbaraka, kinda aliyebuliwa timu ya vijana ya Simba, maarufu Simba B alifunga bao hilo baada ya kumhadaa beki mzoefu, Kevin Yondan na kufumua shuti lililombabatiza beki mwingine wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ na kumpita kipa Deo Munishi ‘Dida’.
  Wakati Kagera bado wapo katika furaha ya bao lao hilo, Mzimbabwe Donald Ngoma akaisawazishia Yanga baada ya shambulizi la haraka akimalizia kwa kichwa krosi ya Simon Msuva dakika ya nne.
  Msuva akafunga mwenyewe dakika ya 21 kuipatia Yanga bao la pili baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa Hussein Sharrif ‘Cassilas’ kufuatia shuti la kiungo Haruna Niyonzima.
  Mzambia Obrey Chirwa akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 26 akimalizia mpira uliotemwa na Casillas tena baada ya shuti la Ngoma.
  Kocha wa Kagera Sugar akampumzisha kipa Cassilas baada ya bao hilo na kumuingiza David Burhan na kipindi cha kwanza kikamalizika Yanga inaongoza 3-1.
  Kipindi cha pili, Kagera wakaanza vizuri na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 49, mfungaji yule yule Mbaraka Yussuf aliyetumia makosa ya mabeki wa Yanga.
  Hata hivyo, Yanga wakaamsha hasira zao na kufanikiwa kupata bao la nne lililofungwa na Deus Kaseke dakika ya 58 kwa shuti akimalizia krosi ya Msuva.
  Chirwa akaifungia Yanga bao la tano akimalizia mpira uliotemwa na kipa Burhan baada ya shuti la Ngoma.
  Donald Ngoma akakamilisha ushindi mnono wa Yanga leo kwa kufunga bao la sita dakika ya 64 baada ya kuambaa na mpira na kumchambua Burhan kufuatia pasi ya Haruna Niyonzima.
  Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Hussein Sharrif ‘Cassilas’/David Burhan dk31, Mwahita Gereza, Godfrey Taita/Babu Ally dk61, Juma Ramadhan, Erick Kyaruzi, George Kavilla, Suleiman Mangoma, Ally Nassoro, Danny Mrwanda, Mbaraka Yussuf na Japhet Makalai
  Yanga SC; Deo Munishi 'Dida', Hassan Kessy/Mbuyu Twite dk53, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent 'Dante', Kevin Yondan, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Obrey Chirwa/Amissi Tambwe dk77 na Deus Kaseke/Matheo Anthony dk79. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAANZA LIGI, WAIPIGA KAGERA 6-2…CHIRWA 2, NGOMA 2, MSUVA MOTO CHINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top