• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 28, 2016

  AZAM FC YAITANDIKA 3-2 KAGERA SUGAR UWANJA WA KAITABA

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  BAO lililofungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 86, limeiwezesha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kuibuka na pointi zote tatu baada ya kuinyuka Kagera Sugar mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba. Bukoba, mkoani Kagera jioni hii.
  Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Azam FC, ulioifanya kupanda kwa nafasi mbili kwenye msimamo baada ya kufikisha jumla ya pointi 19 katika mechi 12 za ligi ilizocheza.
  Mshambuliaji Themi Felix, alianza kuishtukiza Azam FC kwa kuifungia bao la uongozi Kagera Sugar dakika ya 32 kabla ya Mudathir Yahya kusawazisha kwa bao zuri la shuti akimalizia pasi ya kichwa aliyodondoshewa na Bocco kufuatia faulo iliyochongwa na Erasto Nyoni.
  Wachezaji wa Azam FC wakimpongeza Bocco baada ya kufunga bao la ushindi

  Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote zilitoka uwanjani zikiwa nguvu sawa. Kipindi cha pili Azam FC ilikianza kwa kasi kubwa ikitaka kupata bao la uongozi lakini mabeki wa Kagera Sugar walikuwa kizuizi kikubwa kwa washambuliaji wa mabingwa hao wakiokoa hatari zote.
  Mwamuzi wa mchezo wa leo, Mathew Akrama kutoka Mwanza, aliamuru penalti ipigwe langoni mwa Azam FC baada ya beki Aggrey Morris kumfanyia madhambi Ally Nasoro ndani ya eneo la hatari, na penalti hiyo ilifungwa na Felix.
  Baada ya bao hilo, mabadiliko ya wachezaji watatu yaliyofanywa na Kocha Mkuu wa Azam FC kwa nyakati tofauti ya kuwatoa Gonazo Ya Thomas, Gadiel Michael na Jean Mugiraneza na kuingia Shaaban Idd, Frank Domayo na Khamis Mcha,  yaliongeza uhai kwa timu hiyo na kupelekea kufunga mabao mawili yaliyoipa ushindi huo.
  Alianza Domayo dakika ya 80 aliyefunga bao zuri kwa shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 akimalizia mpira uliotemwa vibaya na mabeki wa Kagera Sugar kabla ya Bocco kufunga la ushindi dakika sita baadaye akifunga kwa kichwa safi  kufuatia krosi iliyochongwa na Shaaban Idd.
  Bao hilo linamfanya Bocco kufikisha mabao matano kwenye msimu huu wa ligi akizidiwa mabao mawili na Shiza Kichuya wa Simba, anayeongoza kileleni kwa mabao saba.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael/Khamis Mcha dk 79, Aggrey Morris, Daniel Amoah, Jean Mugiraneza/Frank Domayo dk 70, Ramadhan Singano, Salum Abubakar, John Bocco (C), Mudathir Yahya, Gonazo Ya Thomas/Shaaban Idd dk 62
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAITANDIKA 3-2 KAGERA SUGAR UWANJA WA KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top